Na mwandishi wetu
Kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze anaamini mechi yao na Polisi Tanzania itakuwa ngumu lakini kwa ubora wa kikosi chake anaamini watafanikiwa kuondoka na pointi tatu.
Yanga itakuwa mwenyeji kesho Jumamosi kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu NBC utakaopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam saa 1.00 usiku.
Kaze amefafanua kuwa wanatarajia mchezo mzuri katika kikosi chao kutokana na maandalizi waliyoyafanya ambayo yamekuwa bora zaidi kwa kupata muda wa kupumzika tofauti na mechi zao za mzunguko wa kwanza zilizopita.
Alisema anawaheshimu wapinzani wao kutokana na kiwango walichokionesha kwenye mechi za mwisho za mzunguko wa kwanza, hivyo wana tahadhari zote licha ya wao pia kutaka kutimiza malengo waliyonayo ya kushinda mechi zilizo mbele yao ili wazidi kujikita kileleni.
“Tumewaona Polisi, wamebadilika hasa mechi za mwisho za mzunguko wa kwanza, tunaamini kesho kutakuwa na ushindani mkubwa lakini tumejiandaa vizuri baada ya muda mrefu kupita bila ya kuwa na muda wa kujifua sawasawa kutokana na mechi mfululizo.
“Wachezaji karibu wote wako sawa kiakili na kimwili kitu ambacho hakikuwa hivyo kwenye mzunguko wa kwanza, pamoja na yote tunahitaji alama tatu ili tuanze vizuri raundi ya pili japo tunajua ushindani utakuwa mkubwa sana,” alisema Kaze.
Naye kocha msaidizi wa Polisi, John Tamba ameeleza kuwa wamefanya marekebisho makubwa na maboresho yanayohitajika kuelekea mzunguko wa pili hivyo watahakikisha wanaanza kampeni yao hiyo kwa ushindi.
“Kiufundi tumeiandaa timu vizuri, wachezaji wote wako sawa kimwili na kiakili, tumefanya marekebisho na maboresho kwa mapungufu yaliyojitokeza raundi ya kwanza, tumekuja kivingine kuhakikisha tunapambana kupata matokeo kuanzia kesho na mechi zote zilizobaki,” alisema Tamba.
Yanga inaingia uwanjani ikiwa kileleni kwa pointi 38 ikiwa imefungwa mechi moja katika mechi 15 za ligi zilizopita wakati Polisi ikiwa mkiani kwa pointi tisa ikiwa imeshinda mechi mbili pekee za mzunguko wa kwanza.
Soka Kaze akiri Polisi wagumu lakini…
Kaze akiri Polisi wagumu lakini…
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
