Na mwandishi wetu
Timu ya Singida Fountain Gate imeeleza kuwa inatarajia kwenda nchini Tunisia kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiandaa na msimu ujao wa 2023-24.
Ofisa Habari wa Singida, Hussein Masanza (pichani) ameeleza hayo akifafanua kuwa wanakwenda Tunisia ukiwa ni mwaliko rasmi wa ofa waliyoipata kutoka klabu inayoshiriki Ligi Kuu Tunisia, US Monastir.
“Mipango inakwenda vizuri na panapo maajaaliwa tutaelekea Tunisia, kinachoendelea sasa ni mikakati ya mwisho na maandalizi ya safari hiyo pamoja na kambi kwa ujumla, na siku chache kutoka sasa tutakuwa tumefahamu tarahe ya kuondoka nchini,” alisema Masanza.
Alisema wanalazimika kuwa na maandalizi kabambe kutokana na michuano inayowakabili msimu ujao ikiwemo ya Kombe la Shirikisho Afrika watakayoshiriki kwa mara ya kwanza baada ya kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC.
Aidha, alieleza kuwa wapo kwenye mikakati mizito ya kukisuka kwa ufasaha kikosi chao kwa kutumia falsafa zilizowasaidia katika msimu uliomalizika hivi karibuni ili kufikia malengo waliyonayo.