Na mwandishi wetu
Timu ya Simba SC itacheza mechi mbili za kirafiki ikiwa kambini Dubai, wakianza na Al Dhafrah ya huko na miamba ya Ulaya, CSKA Moscow ya Urusi ambayo imeshiriki michuano ya Uefa na Europa
Wekundu hao waliojichimbia Dubai kwa kambi ya wiki moja ya mazoezi, wataanza kucheza na Al Dhafrah Januari 13 kabla ya kupepetana na CSKA Januari 15, mwaka huu.
Akizungumza na GreenSports, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally ameeleza kuwa kocha wao, Robert Oliveira amefurahishwa na kupata mechi hizo mbili hasa CSKA ambao wamekuwa na ubora na uzoefu mkubwa wa soka.
“Hakuna asiyejua ubora wa CSKA Moscow, ni timu ambayo imekuwa ikishiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kila msimu, naamini ni kipimo kizuri kwa timu yetu na kocha pia ili kujua uimara wa kikosi chake kabla ya kuanza kwa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na mechi za Ligi Kuu,” alisema Ally.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ ameeleza kuwa mchakato wa kusitisha mkataba wa viungo wawili raia wa Nigeria Victor Akpan na Nelson Okwa upo katika hatua za mwisho.
Kiongozi huyo ameeleza kuwa wamezungumza na wachezaji hao na kufikia makubaliano ya kusitisha mikataba na sasa wapo katika hatua za mwisho kuwapa stahiki zao ili waweze kujiunga na timu nyingine zinazowahitaji.
“Nawashukuru kwa uelewa wao wachezaji hawa wameongozwa na busara tangu mazungumzo ya kuvunja mkataba yaanze mpaka hapa tulipofikia kama klabu tunawashukuru na kuwatakia mafanikio huko wanakokwenda,” alisema Try Again.
Kiongozi huyo alisema wachezaji hao si kwamba hawana uwezo bali ushindani uliopo kwenye timu yao ndio imekuwa kikwazo kwao kilichowafanya washindwe kuendana na kasi ya timu yao.
Akpan na Okwa hawakuambatana na timu kuelekea Dubai na kubaki nchini ikielezwa ni kutokana na Umoja wa Falme za Kiarabu kuzuia raia wa Nigeria kupata viza miezi miwili iliyopita na kufafanuliwa kuwa nyota hao wamepewa programu maalumu ya kujifua jijini Dar es Salaam.
Soka Simba kujipima kwa CSKA Moscow
Simba kujipima kwa CSKA Moscow
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
