Paris, Ufaransa
Straika wa Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa, Kylian Mbappe sasa anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji mwenye mabao mengi katika historia ya PSG akifikisha mabao 201 na kumpiku Edinson Cavani.
Mbappe alifikisha bao la 201 jana Jumamosi katika ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Nantes katika mechi ya Ligi 1 akifunga bao la nne kwa timu yake katika dakika za majeruhi.
Baada ya mwamuzi kumaliza mchezo, maofisa PSG walimfanyia sherehe ndogo katika klabu hiyo kuthamini mafanikio yake na sasa rasmi anakuwa mshambuliaji mwenye mabao mengi katika historia ya klabu hiyo.
“Ni jambo la kipekee kuwa hapa, mara ya mwisho nilikuwa hapa wakati natangaza kuendelea kuwa na klabu hii (kuongeza mkataba) na sasa ni heshima kuwa hapa nikiwa mfungaji mwenye mabao mengi,” alisema Mbappe.
Mbappe ambaye ana miaka 24, ameifikia na kuipiku rekodi ya Cavani kwa mechi pungufu, wakati Cavani nyota kutoka Uruguay akifikisha mabao 200 katika mechi 301, Mbappe amefikisha mabao 201 katika mechi 247.
Mbali na PSG, Mbappe pia ni jina kubwa kwenye timu ya Taifa ya Ufaransa akiwa tayari ana Kombe la Dunia alilobeba na timu hiyo mwaka 2018 katika fainali zilizofanyika nchini Urusi.
Kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2022 zilizofanyika Qatar, Mbappe aliibuka mfungaji bora akifunga mabao manane na timu yake kufikia fainali kabla ya kubwagwa na Argentina walioibuka vinara.
.