Manchester, England
Kocha wa zamani wa timu ya Wales, Ryan Giggs amefika mahakamani leo akikabiliwa na kesi ya kumdhalilisha, kumshambulia na kumuumiza aliyekuwa mpenzi wake, Kate Greville na mdogo wake Emma Greville tukio analodaiwa kulitenda Novemba Mosi, 2020 akiwa nyumbani kwake.
Katika kesi hiyo, Giggs pia anatuhumiwa kuwa kati ya Agosti 2017 hadi Novemba 2020 amekuwa na tabia zisizo za kiungwana dhidi ya Kate na tayari amekana kuhusika na tuhuma hizo wakati shauri hilo likitarajiwa kusikilizwa kwa siku 10 mfululizo katika Mahakama ya Manchester.
Giggs ambaye pia ni mchezaji nyota wa zamani wa Man Utd, licha ya kukana kuhusika na tuhuma hizo lakini aliamua kujiuzulu nafasi ya ukocha katika timu ya Wales kwa kile alichodai kwamba asingependa kuona kesi yake inaathiri kwa namna yoyote ile maandalizi ya timu ya Taifa ya Wales kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Doha, Qatar, Novemba mwaka huu.
Tangu akamatwe kwa tuhuma hizo Novemba, 2020, Giggs alijiweka kando na timu ya Wales ambapo mechi yake ya mwisho akiwa na timu hiyo ilikuwa ni dhidi ya Bulgaria katika Nations League, mechi ambayo Wales ilitoka na ushindi wa bao 1-0.
Awali kesi ya Giggs ilikuwa ianze kusikilizwa mwezi Januari lakini ilichelewa sababu ikiwa ni janga la Corona ambapo mahakama ililazimika kubadili taratibu zake za uendeshaji kesi na kulazimika kuahirisha baadhi ya kesi.
Kimataifa Kesi ya Giggs kusikilizwa kwa siku 10
Kesi ya Giggs kusikilizwa kwa siku 10
Read also