Na mwandishi wetu
Timu ya Simba imetozwa faini ya Sh 1,000,000 kwa kosa la mashabiki wake na walinzi wa uwanjani kupanga njama na kufanikisha azma ya kuingia na kufanya vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina.
Tukio hilo linadaiwa kufanywa wakati wa mchezo wao dhidi ya Mashujaa uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.
Adhabu hiyo imetolewa Jumatatu hii baada ya kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) kilichokaa Machi 20, kupitia mwenendo na matukio mbalimbali ya ligi na kufanya maamuzi.
Taarifa hiyo ilisema kuwa mashabiki hao walionekana kupitia video fupi iliyosambaa mitandaoni wakijadiliana na mlinzi wa uwanjani kabla hawajaingia kufanya tukio hilo lililoleta taswira mbaya kwa ligi.
“Walinzi wa uwanjani wa Simba, Kessy Mohamed, Mrisho Mindu, Mohamed Salmin na shabiki Mohamed Saleh, wamefungiwa kuingia viwanjani kwa kipindi cha miezi 12 kwa kosa la kushiriki katika tukio la mashabiki kuingia uwanjani wakati wa mchezo tajwa,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Pia imefafanuliwa kuwa bodi inaendelea na uchunguzi wenye lengo la kufahamu wahusika wengine wa tukio hilo ambao hawakutambulika mara moja ili wachukuliwe hatua kali za kikanuni.
Katika hatua nyingine Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imefuta kadi nyekundu walizooneshwa wachezaji Thomas Ulimwengu wa Singida Fountain Gate na Erasto Nyoni wa Namungo FC baada ya kujiridhisha kupitia ushahidi picha jongeo kuwa hawakustahili adhabu hizo.
Soka Simba yatozwa faini milioni moja
Simba yatozwa faini milioni moja
Read also