Na mwandishi wetu
Kocha wa Simba, Juma Mgunda amesema makosa ya safu yake ya ulinzi ndiyo yaliyosababisha wakashindwa kupata ushindi katika mchezo wa jana Jumatano dhidi ya Mbeya City.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Simba ilitangulia kupata bao dakika ya 14 kabla ya Mbeya City kusawazisha dakika ya 78 matokeo ambayo yameibakisha timu hiyo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo na pointi zao 28.
Kocha huyo amekiri kuwa mchezo ulikuwa mgumu na wenye ushindani mkubwa na hiyo ni kutokana na wenyeji wao Mbeya City kucheza kwa nidhamu na kuwaheshimu muda wote wa mchezo.
“Kabla ya mchezo nilisema mchezo utakuwa mgumu, lakini tulianza vizuri na kupata bao la mapema lakini safu yangu ya ulinzi ilifanya makosa na wenzetu wakapata bao la kusawazisha lakini ndiyo mchezo wa mpira ulivyo, tunakubali matokeo tunarudi uwanja wa mazoezi kujipanga kwa ajili ya mechi zijazo,” alisema Mgunda.
Kocha huyo ameeleza kuwa pamoja na sare hiyo lakini wachezaji wake walipambana kadri ya uwezo wao kutafuta ushindi lakini City walikuwa bora na walifunga njia zote na kujikuta wanamaliza mchezo huo bila kutimiza malengo yao ya pointi tatu.
Mgunda pia aliwapongeza Mbeya City kwa kuonesha ushindani mkubwa kwenye mchezo huo kiasi cha kumuweka katika presha kubwa muda wote wa mchezo.
Kocha Msaidizi wa Mbeya City, Anthoy Mwamlima alisema mchezo ulikuwa mzuri na wenye ushindani mkubwa lakini amehuzunishwa na matokeo ya sare wanayoendelea kuyapata kwenye uwanja wa nyumbani.
“Tunashukuru kwa sare hii lakini lengo ilikuwa ni pointi tatu ukizingatia tulikuwa nyumbani, tumekubali matokeo na tunarudi tena mazoezini ili kurekebisha makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo dhidi ya Simba,” alisema Mwamlima.
Soka Mgunda alaumu mabeki
Mgunda alaumu mabeki
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
