Madrid, Hispania
Mchezaji wa timu ya wanawake ya Hispania, Jenni Hermoso ameiambia mahakama kuwa busu la mdomoni alilopigwa na aliyekuwa bosi wa soka Hispania, Luis Rubiales halikuwa na ridhaa yake.
Mara baada ya timu ya wanawake ya Hispania kuibwaga England na kubeba Kombe la Dunia, Rubiales aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka Hispania alimkumbatia kwa nguvu Jenni na kumpiga busu la mdomoni.
Kitendo hicho kilizua taharuki na kusababisha Rubiales kusimamishwa na Fifa kujihusisha na soka kwa siku 90 kabla ya kuamua kung’atuka nafasi yake katika shirikisho la soka Hispania lakini Jenni aliamua kulifikisha suala hilo mahakamani.
Baada ya mahakama hiyo ya mjini Madrid kuelezwa hivyo na Jenni leo Jumanne, sasa ni jukumu la Jaji kuamua kama Rubiales atashitakiwa kwa kosa la udhalilishaji kijinsia au la.
Jenni, 33, ambaye ni mfungaji kinara wa mabao wa timu ya taifa ya wanawake ya Hispania aliieleza mahakama tukio zima kwa zaidi ya saa moja na vyombo vya habari vilidai kwamba katika hoja zake alisema kuwa busu alilopigwa hakulitarajia na hakukuwa na makubaliano yoyote.
Rubiales kwa upande wake ameshikilia msimamo wake akikana kufanya kosa lolote wakati mahakama imeamua kuendelea na uchunguzi ikiwamo kutumia kamera za CCTV ili kupata ushahidi zaidi wa tukio hilo kabla ya kutoa uamuzi.
Tukio la Jenni kupigwa busu lilitokea Agosti mwaka jana mjini Sydney, Australia mara baada ya mechi ya fainali wakati wachezaji wa Hispania waliobeba taji hilo wakipita jukwaani kuvalishwa medali zao ndipo Rubiales alimpokumbatia Jenni na kumpiga busu la mdomoni.
Kombe la Dunia Kesi ya aliyepigwa busu yanguruma mahakamani
Kesi ya aliyepigwa busu yanguruma mahakamani
Read also