London, England
Kocha wa timu ya taifa ya England, Gareth Southgate (pichani) amelalamikia uwapo wa mfumo wa VAR akidai kwamba umekuwa kero kwa mashabiki wanaokwenda viwanjani.
Maofisa wanaosimamia mfumo wa VAR walishindwa kubadili maamuzi ya bao halali la Liverpool dhidi ya Tottenham Hotspur lililofungwa na Luis Diaz ambalo kimakosa uamuzi uliotolewa ni kwamba mshambuliaji huyo aliotea na mwishowe Liverpool ikalala kwa mabao 2-1.
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ametaka mechi hiyo irudiwe kutokana na makosa hayo ingawa uwezekano wa jambo hilo kukubaliwa ni mdogo mno.
“Kwa wakati wote, tangu nikiwa mtoto mdogo, nimekuwa nikifahamu kwamba uamuzi wa refa ni wa mwisho, unaweza ukubaliane naye au usikubaliane naye lakini tunatakiwa kwenda na hali hiyo,” alisema Southgate.
Southgate hata hivyo alikubaliana na hoja ya kwamba soka haitoweza kuachana na dunia ambayo teknolojia imekuwa ni sehemu ya kufanyia maamuzi.
Kocha huyo hata hivyo akifafanua zaidi kuhusu VAR alisema, “Ninachoweza kusema ni kwamba kila mtu alijikuta akienda katika klabu ya pombe na kulalamika kuhusu mwamuzi, waliendelea kwenda kwenye klabu na kulalamika. Kwa hiyo sina hakika ni kipi hasa ambacho tumekirekebisha.”
“Ninakaa uwanjani pembeni nikiwa na watu wengine, na nina bahati kwa sababu huwa napata tiketi ya bure na baadhi ya watu wanalipa fedha nyingi lakini wanashindwa kuelewa au wanampigia simu mtu aliye nyumbani na kumuuliza kinachoendelea,” alisema.