Berlin, Ujerumani
Ujerumani ndiye mwenyeji wa fainali za Euro 24 lakini timu hiyo inapitia kipindi kigumu na huenda kocha Julian Nagelsmann akatimuliwa kutokana na vipigo anavyoendelea kuvipata katika mechi za kirafiki.
Kipigo cha jana Jumanne cha mabao 2-0 mbele ya Austria ni muendelezo wa vipigo vya timu hiyo chini ya kocha Nageslmann ambaye kabla ya mechi hiyo timu yake ilipoteza mechi dhidi ya Uturuki.
Nagelsmann, kocha wa zamani wa Bayern Munich ambaye ana umri wa miaka 36, alianza kwa ushindi dhidi ya Marekani kabla ya sare dhidi ya Mexico na baada ya hapo hali imekuwa tete dhidi ya Uturuki na Austria.
Kocha huyo ambaye alisaini mkataba Septemba mwaka huu akichukua nafasi ya Hansi Flick ambaye pia alitumuliwa, ana mkataba unaofikia ukomo Julai 2024 baada ya fainali za Euro lakini kwa mwenendo wa timu hiyo huenda asifike wakati huo.
Katika mechi na Austria, bao la kwanza la washindi lilipatikana dakika ya 29 mfungaji akiwa ni Marcel Sabitzer kabla Christoph Baumgartner kumalizia bao la pili dakika ya 73.
Ujerumani pia katika mechi hiyo ilijikuta ikibaki na wachezaji 10 baada ya Leroy Sane, winga wa zamani wa Man City kupewa kadi nyekundu kwa kosa la kumsukuma Phillipp Mwene.
Baada ya matokeo hayo, Nagelsmann alisema kwamba wachezaji wake hawachezi huru na kukiri kwamba bado wana kazi kubwa ya kufanya katika kila eneo la timu hiyo.
“Tunatakiwa kuikubali hali hii lakini hatuwezi kukubali tuwe watu wa aina hii moja kwa moja, tunakuwa vizuri mno kwenye mazoezi lakini hali hiyo haionekani uwanjani siku ya mechi, kuna hali ya kukosa kujiamini jambo ambalo si la ajabu hasa unapoangalia hali ilivyokuwa miezi michache iliyopita,” alisema Nagelsmann.
Nahodha wa timu ya Ujerumani, Ilkay Gundogan, alisema kwamba kilichotokea kinakatisha tamaa hasa kwa kuwa waliwarahisishia wapinzani wao hadi kutengeneza nafasi na kwamba tatizo si ulinzi kwani hata ulinzi unaanzia mbele.
Ujerumani kwa sasa inasubiri kujua wapinzani wake katika fainali za Euro 24 katika makundi ambayo yatatangazwa Desemba 2 ingawa suala la kama Nagelsman ataendelea kuwa na timu hiyo bado lina utata kutokana na matokeo ambayo amekuwa akiyapata.