Kaduguda, Dewji huenda wakaadhibiwa
Na mwandishi wetu
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC, Salim Abdallah ‘Try Again’ amefafanua kuwa iwapo wajumbe wawili wa bodi ya wakurugenzi waliozungumza hivi karibuni kuilaumu klabu hiyo kwenye vyombo vya habari watapatikana na hatia basi hatua stahiki dhidi yao zitachukuliwa.
Hayo yameelezwa baada ya hivi karibuni wajumbe wa bodi hiyo, Mwina Kaduguda na Kassim Dewji kukosoa namna timu hiyo ilivyoshindwa kufanya vizuri msimu huu pamoja na mambo mengine ikiwemo kushutumu baadhi ya viongozi kuyumbisha baadhi ya mambo ndani ya timu hiyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Try Again alisema kwake analiona jambo hilo ni la kuchukiza kwa sababu wajumbe hao wana jukwaa lao la kuzungumzia mambo ya timu, hivyo wana kamati zao za maadili na nidhamu ambazo zitaangalia kama kutakuwa na makosa kwa viongozi hao basi watawachukulia hatua.
“Kuna viongozi wawili wajumbe wa bodi wamekwenda kuzungumza kwenye media mbalimbali, mimi nadhani ni jambo la kuchukiza kidogo, kwa sababu wao wanalo jukwaa la kusema kwa hiyo wasichepuke wabaki njia kuu.
“Ukiwa kiongozi halafu unatoka kwenye bodi unakwenda kuzngumza hadharani kuilaumu klabu unayoiongoza mimi nadhani hiyo si sawasawa, sasa sisi kama bodi tunazo taratibu zetu, tutakaa tutaangalia. Tunazo kamati zetu za maadili, za nidhamu, kama kuna makosa wamefanya basi hatutasita kuchukua hatua, lakin niseme tu kwamba nitoe ombi kwa viongozi waliopo sasa wanayo nafasi ya kushauri si lazima kwenye media, milango yetu iko wazi wakati wowote tuko tayari kupokea ushauri.
“Labda niseme hawa viongozi wawili wapo ndani ya uongozi takriban miaka minne, kwanini mwaka jana hawakusema, mafanikio yaliyopatikana mwaka jana hayawahusu? Sasa iweje haya ambayo wanayaona si mafanikio wawe hawamo, kivipi? Kwa hiyo tukikosea tukosee wote tukipatia tupatie wote, ndiyo dhana bora ya uongozi hivyo niwashauri viongozi wenzangu ni vizuri kushauri lakini njia gani ya kushauri ndiyo tuchague njia bora,” alisema Try Again.
Hali ya Simba kwa sasa inaelezwa kuwa si shwari ndani ya uongozi wa klabu hiyo kutokana na mvurugano wa maneno unaoendelea pia hata kutoka kwa wadau wengine wakubwa wa Wekundu hao.
Miongoni mwa yanayochagiza kwa yanayoendelea sasa ni kutofanya vizuri kwa Simba msimu huu. Ilianza kwa kupoteza Ngao ya Jamii ikifungwa bao 1-0 na Yanga, goli likiwekwa kimiani dakika ya 11 na Fiston Mayele.
Katikati ya msimu, timu hiyo ilifanikiwa kuonesha makucha yake kwa kutwaa ndoo ya Kombe la Mapinduzi ikiifumua Azam bao 1-0 baada ya Meddie Kagere kufunga bao pekee kwa mkwaju wa penalti kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Simba hata hivyo baadaye ilitolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya robo fainali dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwa mikwaju ya penalti 4-3.
Mwendo wa kusuasua kwenye Ligi Kuu ya NBC pia umesababisha kuweka rehani ubingwa waliokuwa wakiutetea dhidi ya Yanga inayoongoza msimamo kwa pointi 64 kwa mechi 26 dhidi ya pointi 51 za Simba wanaoshikilia nafasi ya pili baada ya mechi 25.
Hivi karibuni, Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alitoa taarifa ya kuachana na kocha wao mkuu, Pablo Franco na kocha wa viungo Daniel De Castro ikiwa ni siku chache tangu wavuliwe ubingwa wa Kombe la Azam (ASFC) kwa kufungwa bao 1-0 na Yanga kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
