Na mwandishi wetu
Kampuni ya Azam Media Ltd kwa kushirikiana na klabu za Simba na Yanga zimezindua leo kampeni ya Nani Zaidi baina ya timu hizo zikichuana kwa mashabiki wao katika kuzichangia pesa.
Uzinduzi huo umefanyika kwenye Hoteli ya Serena, Dar es Salaam kwa kuwakutanisha maofisa wa timu hizo ambapo upande wa Simba uliongozwa na Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez na Yanga ni Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingiza.
Baada ya uzinduzi huo ulioelezwa kuwa uchangiaji wake utahesabiwa kama upigaji kura kwa mashabiki hao, Barbara alifafanua kuwa pesa watakazozipata watazipeleka moja kwa moja kwenye ujenzi wa uwanja wao uliopo, Bunju jijini Dar es Salaam ambapo kampeni ya ujenzi wa uwanja huo ilianza tangu Desemba, mwaka jana huku mpaka sasa wakiwa wamefanikiwa kukusanya Sh milioni 60.
“Nieleze kuwa mwezi wa 12 mwaka jana tulianzisha kampeni ya mashabiki kuchangia ujenzi wa uwanja na mpaka sasa tumekusanya milioni 60,” alisema Barbara na kuongeza: “Leo hii mwezi wa sita tunasaini na tumekamilisha kampeni hii mpya na kwa Simba hii ni awamu ya pili.
“Awamu ya kwanza ilikuwa tumeamua tunaweza, hii ya pili ni nani zaidi, kama klabu tunaendeleza ujenzi wetu. Mimi nilisafiri kwenda Doha (Qatar) kwenye mkutano na CAF (Shirikisho la Soka Afrika) na nikazunguka kuona viwanja.
“Mwenyekiti wetu pia Mangungu (Murtaza) mwezi wa pili alienda na kuzunguka Uturuki kuangalia viwanja, mwezi uliopita tumekamilisha mchoro kama klabu na tunajua tukimaliza msimu tutatangaza kile ambacho Simba inakwenda kujenga,” alisema Barbara.

Mazingiza alisema: “Hili jambo ni muhimu sana na mashabiki haifai kukaa pembeni tu kupiga kelele na kisha huendi kuchangia, Yanga ni timu kubwa inapaswa kujiendesha yenyewe kama tulivyoanza kuubadili mfumo wa uendeshaji.
“Kule nyumbani Afrika Kusini kuna Mamelodi Sundowns, Kazier Chiefs na Orlando Pirates hizi klabu zina ushindani mkubwa lakini linapokuja kwenye suala kama hili wanaungana na wanatengeneza pesa nyingi sana, sasa ni wakati wa kuweka pembeni mambo ya ushabiki na kuangalia vitu vya msingi kama hivi, ninapowaona mashabiki wa timu hizi huwa naona pesa.”
Hata hivyo, katika mkutano huo na wanahabari, upande wa Yanga wao walisisitiza kuwa pesa zao katika ushindani huo zitakwenda kwenye mradi wao mwingine ambao watauweka wazi baadaye lakini sio ujenzi wa uwanja.
“Wenzetu wanasema wanapeleka fedha hizi kwenye uwanja sisi tuweke wazi kwamba hatupeleki hata thumni kwenye uwanja, ujenzi wa uwanja wetu ni mradi mwingine na upo katika mchakato hivyo tutakuja na maelezo,” alisema Haji Manara, msemaji wa Yanga.
Kampeni hiyo imezinduliwa rasmi kwa ajili ya watani hao, ikihama kutoka kupambana uwanjani na sasa wafuasi wa timu hizi zamu yao kupambana kuhakikisha mifuko ya timu hizo inatuna kifedha na mwisho kufahamu nani amekuwa juu ya mwingine.
Michango hiyo ambayo inachangwa kupitia namba maalum za mitandao mbalimbali ya simu, pia mwendelezo wake utakuwa ukioneshwa wazi kila siku kupitia program za Azam TV mpaka mwisho wa zoezi hilo.
