Bale aaga rasmi Real Madrid
Winga wa Real Madrid, Gareth Bale leo amewaaga rasmi mashabiki wa timu hiyo huku kukiwa na habari kwamba huenda akaungana na Cristiano Ronaldo katika klabu ya Manchester United.
Bale na Ronaldo wamewahi kuwa pamoja Real Madrid kabla ya Ronaldo kutimkia Juventus na sasa anaichezea timu yake ya zamani wa Man United.
Mkataba wa Bale na Real Madrid unafikia ukomo mwishoni mwa msimu huu na hivyo kuhitimisha miaka yake tisa tangu ajiunge na timu hiyo katika moja ya usajili mkubwa duniani huku mwenyewe akijigamba kwamba ametimiza ndoto iliyokuwa ikimsumbua.
Ronaldo na Bale wamecheza pamoja Real Madrid kwa misimu mitano hadi Ronaldo alipoondoka mwaka 2018 kwenda Juventus na sasa Bale naye anaondoka baada ya kuandamwa na majeruhi na kutokuwa na uhakika wa namba chini ya kocha Carlo Ancelotti.
“Naandika ujumbe huu kuwashukuru wachezaji wenzangu wote wa sasa na wa zamani, makocha wangu, maofisa katika timu na mashabiki ambao wamekuwa wakiniunga mkono, nilikuja hapa miaka tisa iliyopita nikiwa kijana ambaye anataka kutimiza ndoto yake ya kuichezea Real Madrid,” alisema.
“Kuvaa jezi nyeupe, kuvaa fulana ya mazoezi kifuani kwangu, kucheza uwanja wa Santiago Bernabeu, kutwaa mataji na kuwa sehemu ya kitu maarufu hadi sasa, kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, kwa sasa naweza kuangalia nyuma na kuvuta picha na kisha nikasema ama hakika ndoto hii imekuwa kweli pamoja na mambo mengine mengi.”
Bale pia amewahi kuwa mchezaji muhimu na kipenzi cha mashabiki wa timu ya Tottenham na mbali na Man United, mchezaji huyo pia anahusishwa na mipango ya kurudi kwenye timu yake hiyo ya zamani.
Akiizungumzia Tottenham na jinsi alivyoondoka katika timu hiyo, Bale anasema, “Nashukuru kwa kila kitu ambacho nilifanyiwa, lakini najua pia walielewa wakati ule kwamba inapotokea klabu kubwa kama Real Madrid kukutaka ni vigumu kukataa, ingawa nilifurahia maisha yangu pale Tottenham, nilipendwa na bado napendwa lakini inapokuja Real Madrid kwako ukiikataa utajuta.”
Bale na Ronaldo licha ya kutofautiana wakiwa Real Madrid lakini wamekuwa marafiki wazuri na hata Ronaldo aliporudi kwa mara ya pili Man United, Bale alitumia mitandao ya kijamii kumtakia kila la lakheri huku akiamini atafanya vizuri.
Mbali na Man United na Tottenham, klabu nyingine inayohusishwa na mipango ya kumsajili Bale ambaye kwa sasa yuko na kikosi cha timu ya Taifa ya Wale, ni Cardiff City huku pia ikidaiwa kwamba huenda akaenda kucheza soka Marekani.
