Azam yahitaji muda kutimiza malengo
Na mwandishi wetu
Azam imeeleza kuhitaji muda ili kukamilisha mipango waliyoanza nayo tangu kuanza kwa msimu ili kuifanya iwe tishio na kutimiza matamanio ya wengi wanaoifuatilia.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Soka wa Azam, Jonas Tiboroha wakati akijibu hoja za kwa nini Azam inaonekana ina uwezo mkubwa kifedha na hata wachezaji lakini inashindwa kuonesha makali yao stahiki.
“Si kwamba timu haitaki mafanikio kama ambavyo watu wanafikiria lakini hili ni suala la mchakato ambao hata mimi nimeukuta wakati naanza kazi mapema msimu huu, safari hii tumetengeneza mfumo ambao utatusaidia kutoka hapa.
“Kwa sasa siwezi kuongea sana kwamba tulikuwa tunafeli wapi maana itakuwa kama tunauza mipango yetu kwa wapinzani lakini niwaambie haya maswali tukiulizwa tena msimu ujao tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuyajibu ila sasa tupewe muda,” alisema Tiboroha.
Azam ambayo inaelezwa kuwa klabu tajiri nchini kutokana na namna inavyohudumia wachezaji kisasa na uwepo wa vitendea kazi vya kutosha kwa timu ya Ligi Kuu lakini imeambulia ubingwa wa ligi mara moja pekee msimu wa 2013-14 tangu ilipopanda mwaka 2007.
Kuhusu msimu huu kuhangaika kutafuta nafasi nne za juu ambazo zinaonekana kuwa ngumu kwao, Tiboroha alisema wanahisi hawana bahati msimu huu kwa sababu wachezaji wao wengi tegemeo wamekuwa wakiumia na kukaa nje kwa muda mrefu.
Azam kwa sasa ipo nafasi ya nne kwa pointi 37 sawa na Namungo inayoshika nafasi ya tatu wakipishana mabao ya kufunga na kufungwa. Azam pia inapata upinzani mkubwa kutoka kwa Geita Gold inayoshikilia nafasi ya tano ikiwa na pointi 36.
“Kilichopo sasa tunahitaji kupambana kumaliza kwenye nafasi hizo nne za juu ili tupate nafasi ya kimataifa maana tofauti na hapo hiyo haiwezi kuwa hadhi ya Azam kwamba ishiriki tu ligi ya ndani bila ya kushiriki kimataifa,” alisema Tiboroha.
