Na mwandishi wetu
Baada ya uongozi wa Yanga jana kutangaza kuachana na mshambuliaji wake, Saido Ntibazonkiza, wachezaji wenzake wa timu hiyo wamemtakia kila la heri mchezaji huyo huko aendako.
Yanga ilitangaza hatua hiyo ikieleza kuwa mchezaji huyo amemaliza mkataba wake na timu hiyo, hivyo wanamtakia kila la heri baada ya kipindi cha miaka miwili alichoitumikia timu hiyo tangu alipotua Jangwani akitokea Vital’O ya kwao Burundi.
Kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii, Aboubakar Salum ‘Sure Boy’ aliandika: “Kila la heri kaka, Mungu akufanyie wepesi kwenye kila hatua mtu safi.” Yacouba Songne aliandika kwa kifupi: “Kila wakati, wakati mwingine kaka.”
Kipa wa Yanga, Abdultwalib Msheri aliyetua Yanga hivi karibuni akitokea Mtibwa Sugar naye alimtakia kila la heri kwa kuandika: “Kila la heri kaka, Baba wa Bujumbura.”
Ikumbukwe kuwa Saido ambaye mkataba wake umeisha Mei 30, mwaka huu alikosekana kwenye mechi ya mwisho ya Yanga waliyoc
heza nusu fainali ya Kombe la Azam (ASFC) na kuifunga Simba bao 1-0, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Saido na Dickson Ambundo walienguliwa kwenye kikosi hicho cha Nasreddine Nabi kwa makosa ya utovu wa nidhamu ikielezwa walirejea kambini alfajiri bila ya ruhusa maalum kisha kuelezwa kuwa hatma yao itafahamika baada ya mechi hiyo ya Simba.
Pamoja na hayo, duru mbalimbali za michezo zinabainisha kuwa mshambuliaji huyo aliyefunga mabao saba na kutoa asisti nne kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu, anawindwa na klabu maarufu nchini na pengine msimu ujao anaweza kuonekana kwenye ligi hiyo akiwa na jezi tofauti.
Soka Wachezaji Yanga wamuaga Saido
Wachezaji Yanga wamuaga Saido
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
