Paris, Ufaransa
Liverpool na Real Madrid leo zinaumana katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mechi ambayo kila timu itaingia uwanjani ikisaka rekodi ya kutwaa mataji matatu katika msimu mmoja.
Liverpool tayari imebeba Kombe la FA na lile la Ligi wakati Real Madrid wana taji la Ligi Kuu Hispania au La Liga pamoja na lile la Mfalme hivyo rekodi ya taji la tatu ni mtihani ambao watapenda kuukamilisha usiku wa leo jijini Paris, Ufaransa.
Real Madrid ndiye mbabe wa taji hilo akiwa anaongoza kwa kulibeba mara 13 wakati Liverpool wao wanawania taji la saba na wakifanikiwa watakuwa sawa na AC Milan ambayo inashika nafasi ya pili kwa kulitwaa taji hilo mara nyingine.
Liverpool bado wana kumbukumbu ya kulikosa mwaka 2018 mbele ya Real Madrid walipolala kwa mabao 3-1 katika mechi ya fainali.
Kumbukumbu hizo bado hazijawatoka baadhi ya wachezaji wa Liverpool mmoja wao akiwa ni Mohamed Salah, mshambuliaji tegemeo wa timu hiyo ambaye umuhimu wake katika mechi ya leo hauwezi kuwekwa pembeni.

Kwa Salah mechi hiyo ilikuwa ngumu na mbaya, alitoka dakika ya 30 akiwa analia baada ya kuumia bega la kushoto wakati akipambana na beki mbabe wa Real Madrid, Sergio Ramos, hivyo usiku wa leo utakuwa na maana kubwa kwani atakumbuka alivyowakosa Madrid katika fainali hiyo.
“Nataka kucheza dhidi ya Real Madrid na pia nataka kushinda dhidi yao,” alisema Salah akizungumzia mechi yao ya leo na Real Madrid.
Ukimzungumzia Salah hapo hapo utalazimika kumzungumzia mshambuliaji wa Real Madrid, Karim Benzema ambaye kama ilivyo kwa Salah, leo naye ni mtu muhimu katika kuhakikisha Real Madrid wanaendeleza rekodi yao ya kibabe katika michuano hiyo mikubwa ya klabu barani Ulaya.
Benzema ameiwezesha Real Madrid kutwaa taji la La Liga akiwa kinara wa mabao wa ligi hiyo baada ya kutupia kambani mara 27, Salah naye ni kinara wa mabao Ligi Kuu England akiwa anaongoza kwa kufunga mabao 23, tofauti yao ni kwamba Benzema ameipa taji la La Liga Real Madrid jambo ambalo Salah ameshindwa ingawa hilo haliondoi umuhimu wa Salah katika kuzifumania nyavu.
Kiasili wachezaji wote hawa ni waafrika, Benzema ni Mfaransa mwenye asili ya Algeria wakati Salah ni mzaliwa na raia wa Misri. Benzema ana miaka 34 akiwa amemzidi Salah miaka mitano.
Tofauti hiyo ya umri pia inajidhihirisha katika mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Benzema amelibeba taji hilo mara nne akiwania kulibeba mara ya tano usiku wa leo wakati Salah ana taji moja akiwania taji la pili usiku wa leo.
Benzema pia ndiye kinara wa mabao Ulaya akiwa na mabao 15 huku akitajwa kuwa katika nafasi nzuri ya kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia.
Ukija kwa makocha Carlo Ancelotti wa Real Madrid ana miaka 62, akimzidi Jurgen Klopp wa Liverpool kwa miaka minane, tofauti ambayo pia inajidhihirisha katika rekodi zao za kulibeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika rekodi hizo, Ancelotti yuko mbali akiwa amebeba mataji hayo mara tatu, mbili na AC Milan na mara moja na Real Madrid hivyo leo usiku anawania taji la nne na akilibeba atakuwa amefanya hivyo mara ya pili na Real Madrid na hivyo kuwa mara mbili na AC Milan na mara mbili na Real Madrid.
Klopp yeye tayari amebeba taji hilo mara moja akiwa na Liverpool na leo atakuwa akiwania kulibeba mara ya pili akiwa na timu hiyo hiyo, hakuwahi kufanya hivyo hapo kabla na timu yoyote nyingine.
