Manchester, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag anapambana kuwatuliza wachezaji tegemeo ambao wanaonekana kutoridhishwa na mambo yanavyokwenda baada ya kufungwa bao 1-0 na Newcastle ikiwa ni kipigo cha 10 msimu huu.
Baadhi ya wachezaji wako pamoja na Ten Hag na wasaidizi wa kocha huyo lakini kuna hofu katika klabu hiyo kwamba hali kwenye vyumba vya kubadilishia nguo itazidi kuwa tete kama mambo hayatanyooka haraka.
Mwenendo wa Man United kwa sasa hauridhishi na hali huenda ikawa mbaya zaidi kwa kuwa timu hiyo inakabiliwa na ratiba ngumu katika wiki mbili zijazo, itakuwa na mechi dhidi ya Chelsea, Bayern Munich na Liverpool.
Miongoni mwa mambo ambayo inadaiwa wachezaji wamekuwa wakiyajadili ni ugumu unaokuwapo katika vipindi vya mazoezi ya kocha huyo tangu wakati wa ziara ya maandalizi ya msimu nchini Marekani.
Pia mbinu za Ten Hag zimekuwa zikijadiliwa hasa baada ya timu hiyo kujikuta ikiruhusu sare ya mabao 3-3 dhidi ya Galatasaray na kipigo cha bao 1-0 mbele ya Newcastle.
Kwa upande wake Ten Hag inadaiwa kuwa amekuwa akijitahidi kuwatuliza wachezaji wake ili kuleta hali ya utulivu ikiwamo kuwatetea mchezaji mmoja mmoja licha ya kucheza chini ya kiwango au kufanya makosa ya wazi.
Hivi karibuni, kocha huyo alikataa kumlaumu kipa Andre Onana kwa makosa aliyoyafanya katika mechi na Galatasaray na pia alimtetea mshambuliaji wake Marcus Rashford licha ya kutocheza vizuri katika mechi na Newcastle.
Habari za ndani zinadai kuwa baadhi ya wasaidizi wa Ten Hag wanafahamu kuwa kuna wachezaji ambao hawapendi namna wanavyoshutumiwa hadharani mambo yanapoharibika.
Wachezaji ambao wanatajwa kuweza kumpa msaada Ten Hag ili kutuliza mambo kwenye vyumba vya kubadilishia nguo ni Lisandro Martinez na Casemiro ambao wote kwa sasa ni majeruhi.
Wakati yote hayo yakiendelea uwekezaji wa tajiri mpya, Sir Jim Ratcliffe anayetarajia kununua hisa asilimia 25 unasubiriwa kwa hamu ingawa pia umeibua hali ya wasiwasi kuhusu majaliwa ya watendaji kadhaa ndani ya klabu hiyo.
Kimataifa Ten Hag ahaha kutuliza wachezaji
Ten Hag ahaha kutuliza wachezaji
Read also
