Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imeleezea kilichotokea hadi kuwasimamisha wachezaji wao wawili, Saido Ntibazonkiza na Dickson Ambundo na kufafanua kuwa watakuwa nje ya timu hiyo mpaka watakapokutana na kocha Nassredine Nabi kuzungumza kilichotokea.
Ntibazonkiza na Ambundo waliondolewa kwenye kambi ya timu hiyo mkoani Shinyanga juzi wakati Yanga ikijiandaa na mchezo wao wa nusu fainali wa Kombe la Azam (ASFC) kwa kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu.
Ofisa Habari wa Yanga, Haji Manara amefafanua kuwa wachezaji hao walimchukiza Nabi baada ya kutoroka kambini baada ya mchezo wao dhidi ya Biashara United na kurejea alfajiri na hivyo kuenguliwa kwa sasa mpaka watakapomaliza kibarua chao dhidi ya Simba.
“Kocha Nabi ameamua kuwasimamisha Saido na Ambundo kwa wiki hii na baadaye wakija Dar es Salaam watazungumza naye na uongozi kuona nini kitaendelea, ni kweli Sadio na mwenzake mara baada ya mechi yetu na Biashara waliondoka kambini na kurudi alfajiri.
“Kitendo hicho kimemfadhaisha kocha na uongozi wa klabu kwa ujumla wameamua kuwasimamisha kupisha kwanza mechi hii na kuleta morali kwenye timu. Nabi amefanya hivi ili ijulikane Yanga ni klabu ya watu, wachezaji na mashabiki wote na itakuwa si jambo jema kwa tukio kama lile na kuendelea kukaa na wachezaji hao kambini,” alisema Manara.
Kukosekana kwa wachezaji hao kuelekea mechi hiyo kumeibua wasiwasi kwa mashabiki wa Yanga kutokana na viwango vilivyooneshwa na wachezaji hao hivi karibuni.
Ambundo ameifungia Yanga mabao mawili kwenye mechi tatu za mwisho alizoanza kikosi cha kwanza wakati Ntibazonkiza akiwa ndiye mfungaji bora wa pili wa timu hiyo baada ya Fiston Mayele, akiwa amefunga mabao saba na kutoa asisti nne.
Manara amewataka mashabiki wa timu hiyo kutofadhaishwa na kinachoendelea kwa kukosekana kwa wachezaji hao kwani wamesajili wachezaji wengi wenye uwezo wa kuwapa matokeo kwenye mchezo wao huo utakaopigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Soka Hatma ya Ambundo, Saido anaijua Nabi
Hatma ya Ambundo, Saido anaijua Nabi
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
