London, England
Jumapili Mei 22, kati ya saa moja na nusu hadi saa mbili kinara wa Ligi Kuu England atakuwa kajulikana. Swali ni je atakuwa Liverpool au Man City?
Je atafurahi kocha Mhispania, Pep Guardiola wa City au Mjerumani, Jurgen Klopp wa Liverpool? Nani hesabu zitamuendea vizuri? Yote hayo yatajulikana kati ya saa moja na nusu hadi saa mbili.
Ligi Kuu England inafikia tamati Jumapili hii kwa timu zote 20 kujitupa uwanjani, maana yake ni kwamba ligi hiyo inahitimishwa kwa mechi 10, kati ya hizo fikra za mashabiki wengi zitakuwa katika mechi kati ya Liverpool na Wolves na City na Aston Villa, mechi ambazo matokeo yake ndiyo yatakayoamua nani anakuwa bingwa kwa msimu huu wa 2021/22.
City ndiyo inayoshika usukani wa ligi hiyo ikiwa na pointi 90 wakati Liverpool inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 89, hivyo timu yoyote kati ya hizo ili kujihakikishia ubingwa wa ligi hiyo ni lazima ishinde mechi yake ya mwisho au mechi ya Jumapili.
Tofauti ya pointi moja katika mechi ya mwisho inaweza isiwe na maana yoyote kwa City kama timu hiyo itapoteza au kutoka sare mechi yake ya mwisho na Liverpool akashinda.
Ule msemo wa kila timu inatakiwa kushinda ndio unaotumika katika mechi za leo baina ya vigogo hao wa England, inaweza kuwa faida kwa City iwapo wao watapoteza na Liverpool kupoteza ingawa hakuna kocha au timu inayoweza kuingia uwanjani na mahesabu hayo hasa katika mechi ya mwisho, hesabu pekee ya kulisaka taji hilo ni kushinda mechi ya leo.
Unaweza pia kuangalia mabao 96 ya kufunga waliyonayo City na 91 ya Liverpool na kusema kwamba City wana faida ya mabao kwamba hata wakifungwa na Liverpool kutoka sare idadi hiyo ya mabao kimahesabu inaweza kuwa na maana kwenye mbio za ubingwa lakini ukweli unarudi pale pale kwamba hakuna timu itakayoingia uwanjani kwa mechi ya mwisho na kuanza hesabu za sare au kutegemea mpinzani wako katika mbio za ubingwa kufungwa.
Nje ya hesabu hizo, Liverpool wapo katika mkakati wa kuweka rekodi ya aina yake England ya kubeba mataji manne katika msimu mmoja, tayari wana taji la FA na la Ligi, wakifanikiwa kulibeba taji la LigiKuu England, kazi ya mwisho ya kuweka rekodi hiyo itakuwa kubeba taji la nne ambalo ni taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo Mei 28 watakuwa jijini Paris kuumana na Real Madrid.
Mechi za mwisho England pia zinapambwa na vita ya kusaka nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, ziweke kando Liverpool na Man City, hizo zimeshafuzu, hapo hapo iongeze na Chelsea na mtihani unabaki kati ya mahasimu wa London, Tottenham na Arsenal, nani atashika nafasi ya nne kuungana na timu tatu za juu.
Arsenal ina pointi 66 na Tottenham 68, kama ilivyo kwa Man City na Liverpool nao ushindi unawahusu, Tottenham licha ya kuwa na faida ya pointi lakini ikipoteza mechi na Norwich na Arsenal ikambwaga Everton, Tottenham wanakuwa wameikosa nafasi ya nne.
Hapo hapo pia kuna mbio za kusaka tiketi ya michuano mingine midogo ya Ulaya lakini hilo liweke kando, ipo vita ya kupambana kujinasua na janga la kushuka daraja na hivyo kuikosa Ligi Kuu England msimu ujao, nako kuna kazi. Watford na Norwich tayari zimetangulia kazi sasa ipo kwa Leeds na Burnley, kila moja ina kazi ya kucheza hesabu zake vizuri katika mechi yake ya mwisho ili ibaki Ligi Kuu England msimu ujao.
Mtihani wao pia ni mgumu kwani timu zote zina pointi 35 ingawa Burnley wana faida ya kufungwa mechi chache na mabao machache ukilinganisha na Leeds lakini ugumu uko pale pale atakayetoa sare atashuka iwapo mwenzake atashinda, atakayetoka sare hatoshuka iwapo mwenzake atashindwa.
Mechi zote za leo ambazo zitachezwa saa 12 jioni ni kama ifuatavyo…
Liverpool v Wolves
Man City v Aston Villa
Chelsea v Watford
Brentford v Leeds
Arsenal v Everton
Leiceter v Southampton
Norwich v Tottenham
Brighton v West Ham
Crystal Palace v Man United
Burnley v Newcastle
