Na mwandishi wetu
Baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam, Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco amekiri kuwa ulikuwa mchezo mgumu kwa timu zote mbili japo walijaribu kucheza vizuri kuwafurahisha mashabiki waliojitokeza lakini mambo hayakwenda walivyotarajia.
Katika mchezo huo uliopigwa jana usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Azam ilikuwa ya kwanza kandika bao dakika ya 38 kupitia kwa Rogers Kola huku Simba ikisawazisha dakika ya 45, bao lililofungwa na John Bocco.
Sare hiyo imeifanya Simba kufikisha pointi 50 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na kufanya pengo baina yao na Yanga iliyo kileleni kuwa pointi 10 huku kila timu ikiwa imeshacheza mechi 24.
Pablo raia wa Hispania alisema kuwa mara nyingi mchezo wa Simba na Azam umekuwa mgumu, kwani hata ukiangalia matokeo ya michezo iliyopita miaka mitano nyuma utagundua kuwa ni mechi ngumu sana kushinda dhidi yao.
“Mchezo ni mgumu, ilitarajiwa hivyo lakini kumekuwa na utofauti zaidi ila bado tumebakiwa na michezo sita ya ligi ambayo tunapaswa kupambana na kupata matokeo ya ushindi ili kujiweka katika nafasi na mazingira mazuri kwenye msimamo,” alisema Pablo.
Kocha wa Azam, Abdihamid Moallin alisema kuwa wakati wanaingia kuikabili Simba walikuwa wanajua utakuwa mchezo mgumu hivyo walijipanga kuhakikisha wanapata ushindi lakini wamepata sare hivyo sasa wanaangalia mchezo ujao.
“Ulikuwa mchezo mgumu, tulijaribu kutengeneza nafasi za kufunga tukashindwa kuzitumia, baadaye tulipoteza kitu kwenye eneo la ushambuliaji baada ya kutoka Rodgers Kola ingawa Shaban Idd aliyeingia ni mchezaji mzuri lakini ametoka kwenye majeruhi ingawa alionesha kiwango safi.
“Hivi sasa tunaachana na mchezo huu uliopita na sasa tunaangalia mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa Manungu, tunakwenda kujiandaa dhidi yao,” alisema Moalin.
Sare ya mchezo huo inakuwa sare ya 10 baina ya timu hizo katika mechi 28 za Ligi Kuu Bara walizokutana hadi sasa. Simba imeshinda mara 13 wakati Azam imeshinda katika mechi tano.
Soka Mechi ilikuwa ngumu-Makocha Simba, Azam
Mechi ilikuwa ngumu-Makocha Simba, Azam
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
