Na mwandishi wetu
Timu ya Yanga imeweka kambi jana tayari kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Mbeya Kwanza unaotarajiwa kupigwa kesho katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Yanga ambayo imebakiza michezo sita ikiwania pointi 12 kwa ajili ya kujihakikishia ubingwa msimu huu imesema inatambua ugumu wa mchezo huo kutokana na mazingira ya timu wanayocheza nayo inayopambana isishuke daraja.
Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amefunguka kuwa wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanapata matokeo ya ushindi katika mechi hiyo ili wazidi kuukaribia ubingwa mapema huku akisisitiza mashabiki kujitokeza kwa wingi katika mechi hiyo ili kuongeza hamasa ya ushindi siku hiyo.
“Timu leo (jana) imeingia kambini kwa maandalizi baada ya kumaliza mechi yetu na Dodoma Jiji na tunatambua ugumu wa mchezo wenyewe kutokana na mazingira ya timu tunayocheza nayo, mara nyingi timu zinazopambana zisishuke daraja huwa zinapambana kweli kwenye mechi kama hizi.
“Ni kama vile tulipocheza na Tanzania Prisons ambao nao wako mkiani lakini tulitoka nao suluhu kwa hiyo kwa mazingira hayo mechi itakuwa ngumu lakini mashabiki tujitokeze kwa wingi kwa ajili ya mchezo huo kwa ajili ya kuwasapoti vijana wetu na kuhakikisha timu inapata matokeo,” alisema Bumbuli.
Mbeya Kwanza ambayo inaburuza mkia kwa pointi 23 baada ya mechi 21 imepoteza michezo yake miwili iliyopita hivyo sasa inapambana kuhakikisha inapata pointi kwenye mechi zake saba zilizosalia ili ing’atuke mkiani.
Upande wa Yanga ambayo mechi yake ya mwisho iliifumua Dodoma Jiji kwa mabao 2-0 yenyewe ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa pointi 60 baada ya mechi zake 24, Simba inaifuatia ikiwa na pointi 49 baada ya mechi 23 na leo usiku inatarajia kuumana na Azam kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Soka Yanga yaipigia hesabu Mbeya Kwanza
Yanga yaipigia hesabu Mbeya Kwanza
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
