Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele amesema kuwa anachopitia sasa ni changamoto ya mchezo wa soka lakini hajakata tamaa, bado anapambana kuhakikisha anatwaa kiatu cha ufungaji bora mwishoni mwa msimu huu.
Mayele amezungumza hayo ikiwa ni mechi ya nne mfululizo sasa sawa na dakika 360, mshambuliaji hajafunga bao na kuibua hofu kwa mashabiki wa timu hiyo kuhusu upatikanaji wa mabao mengi kwa mechi zilizosalia ili watimize ndoto yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Mayele ameeleza kwamba changamoto kama hizo huwa zinatokea kama vile ambavyo ilitokea pia kutopata matokeo kwenye mechi tatu mfululizo kabla ya juzi kuifumua Dodoma Jiji kwa mabao 2-0, hivyo na yeye pia atakaa sawa na ataendelea kukipigania kiatu hicho.
Mpaka sasa Mayele amefunga mabao 12 akizidiwa bao moja na kinara George Mpole wa Geita Gold ambaye ameongeza idadi hiyo kwa kufunga bao moja kwenye ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya Kwanza.
“Nashukuru Mungu tumeanza kupata ushindi baada ya zile sare zilizopita, ni kweli kwa sasa sijafunga muda lakini magoli yatakuja tu yenyewe maana hiyo ni changamoto ya mpira lakini malengo makubwa ni kutwaa ubingwa, malengo ya timu ndiyo namba moja siku zote.
“Kisha baada ya hapo ndiyo yanakuja malengo ya pili, malengo yangu binafsi ya kuendelea na mbio zangu za kutwaa kiatu, bado mechi sita tunahitaji ushindi na mimi nitaendelea kufunga niendelee kutetema, kwenye hizi mechi mabeki wananikaba sana na hiyo inanipa nguvu mimi ya kuendelea kupambana kuitafutia timu ushindi,” alisema Mayele.
Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya NBC kwa pointi 60 baada ya mechi 24, Simba inafuata ikiwa na pointi 49 kwa mechi 23. Yanga imesaliwa na mechi sita kabla ya kumalizika kwa ligi dhidi ya timu za Mbeya Kwanza, Biashara United, Coastal Union, Polisi Tanzania, Mbeya City na Mtibwa Sugar.
Na Yanga inahitaji ushindi wa mechi nne pekee ambazo ni sawa na pointi 12 kujihakikishia ubingwa kwa kuwa hakuna timu itakayofikia pointi hizo.
Soka Mayele ajipa matumaini, Mpole amzidi mabao
Mayele ajipa matumaini, Mpole amzidi mabao
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
