Na mwandishi wetu
KLABU ya Simba imedai kuwa kabla ya kuzungumzia faini waliyopigwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwanza wanahitaji kusikia majibu juu ya malalamiko yao kuhusu timu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini ilipokuja kucheza dhidi yao.
Simba imepigwa faini ya Dola za Marekani 10,000 (sawa na Sh milioni 23) kwa kosa la kuwasha moto katikati ya uwanja uliokuwa umezungukwa na wachezaji wa timu hiyo dakika chache kabla ya kuanza kwa mchezo wa pili wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika uliopigwa Aprili 24 mwaka huu, Uwanja wa Orlando Pirates.
Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu amesema kwamba kwa sasa hana la kuzungumza kuhusiana na adhabu hiyo lakini zaidi na wao pia wanataka kujua kwanza kuhusu malalamiko yao kwa Orlando baada ya kuripoti kuhusu vitendo ukiukwaji taratibu vilivyofanywa na Orlando.
“Sawa inawezekana ikawa imesemwa hivyo lakini hata sisi pia yapo ambayo tumeyalalamikia na bado hawayajayatolea mamuzi kwa hiyo nadhani nipitie hayo maamuzi, tuone yale ambayo na sisi tuliwaandikia wamesema nini.
“Kwa sababu hata wao hapa walikuja wakaruka ukuta, wakapita njia ambazo haziruhusiwi kwa hiyo ni mambo ambayo yanafanya tuendelee kufanya mawasiliano na CAF halafu tutatoa kauli. Tutaangalia kwanza maudhui yenyewe na tangu tumerudi hapa hatujakaa kufanya tathmini, ni jambo la kusubiria tuone jinsi gani tutalitolea taarifa hilo jambo,” alisema Mangungu.
Simba ambayo ilipoteza kwa penalti 4-3 katika mchezo huo baada ya ushindi wa bao 1-0 kwa kila timu ikiwa nyumbani, iliadhibiwa na CAF kwa kilichoelezwa ni kufanya tambiko hatarishi uwanjani.
Kabla ya hukumu hiyo, CAF ilisikiliza hoja za pande zote husika na kuzichambua video na picha zilizoonesha tukio hilo na kujiridhisha juu ya utoaji wa hukumu hiyo ambayo Simba imepewa fursa ya siku tatu ya kukata rufaa au vinginevyo kutekeleza adhabu ya kulipa fedha hizo ndani ya siku 60.
Kimataifa Simba yaigeuzia kibao CAF
Simba yaigeuzia kibao CAF
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
