Paris, Ufaransa
Kifo cha aliyekuwa mshambuliaji Nice, Emiliano Sala kimewaibua viongozi wa klabu hiyo ambao wamewashutumu baadhi ya mashabiki wao kwa kufanyia dhihaka kifo cha mshambuliaji huyo.
Sala, raia wa Argentina alifariki kwa ajali ya ndege Januari, 2019 wakati akielekea Uingereza kukamilisha usajili wake na klabu ya Cardiff City lakini jana Jumatano baadhi ya mashabiki wa Nice walisikika wakiimba nyimbo za kudhihaki kifo cha mchezaji huyo katika mechi yao na Saint-Etienne ambayo walishinda kwa mabao 4-2.
Tukio hilo limewakera viongozi wa Nice hasa kwa namna ambavyo zomea zomea hiyo na nyimbo za
ajabu zilivyokuwa zikimhusisha mchezaji huyo wa zamani wa Nice ambako baadhi ya mashabiki hao walisikika wakisema kuwa Sala ni Muargentina ambaye hajui kuogelea.
Mei 7 mwaka huu Nice walipoteza mechi ya fainali ya Kombe la Ufaransa kwa Nantes ndipo mashabiki hao pengine wakatumia ushindi wao na Etienne kujipoza kwa namna mbaya ya kudhihaki kifo cha Salaaliyefariki dunia akiwa na miaka 28 ambaye msimu uliopita aliichezea Nice, timu ya Ligi 1.
Taarifa ya Nice kuhusu tukio hilo ilisema, “Nice tunashutumu kwa nguvu zote zomea zomea zilizomhusu Emiliano Sala Jumatano jioni pale Allianz Riviera. Klabu hiyo pia imefafanua kuwa iko pamoja na inaungana na familia na marafiki wa Emiliano Sala.”
Kocha wa Nice, Christophe Galtier naye aliwashutumu wote waliohusika na tukio hilo aliposema, “sina namna ya kuelezea nilichokisikia, tunapenda kuomba msamaha kwa familia ya Emiliano Sala.”
Nantes nao katika taarifa yao walieleza kuguswa na tukio hilo lililofanywa na baadhi ya mashabiki wa
timu ya Nice na inalaani kwa nguvu zote tabia hiyo ambazo zinadhihaki kumbukumbu ya Emiliano Sala.
Naye kocha wa timu hiyo, Antoine Kombouare aliongeza, nimechukizwa, watu hawa hawana nafasi kwenye viwanja vya soka, wanatakiwa kufungia, naisikitikia familia ya Sala.
