Madrid Hispania
Karim Benzema, jana usiku alidhihirisha umahiri wake alipoisaidia Real Madrid kufuzu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Man City.
Benzema ndiye aliyefunga bao la ushindi kwa mkwaju wa penalti na kutoa pasi iliyozaa bao la kwanza na kupata ushindi ambao sasa utawakutanisha na Liverpool katika mechi ya fainali itakayopigwa Mei 28 jijini Paris, Ufaransa.
City ndio waliokuwa na matumaini makubwa ya kucheza fainali hiyo kutokana na ushindi wa mabao 4-3 walioupata katika mechi ya nusu fainali ya kwanza kabla Benzema hajawaharibia siku jijini Madrid na kuifanya City itolewe katika michuano hiyo kwa jumla ya mabao 6-5.
Wakiwa ugenini City waliuanza vizuri mchezo wa jana wakicheza kwa umakini, kujihami na kushambulia na haikushangaza walipopata bao la kwanza katika dakika ya 73 lililofungwa na Mahrez akiitumia vizuri pasi ya Bernado Silva.
Bao hilo lilizidi kuyabeba matumaini ya timu hiyo lakini mambo yalianza kuwaendea kombo katika dakika ya 89 kwa bao lililofungwa na Rodrigo kwa shuti la kiufundi la mguu wa kushoto akiitumia vizuri pasi ya Benzema.
Wakati dakika 90 zikikaribia kutimia, dakika 6 za nyongeza zilikuwa neema kwa Real ambao waliandika bao la pili dakika moja baadaye, bao lililofungwa na Rodrigo tena safari hii kwa kichwa akiitumia pasi ya Asensio na hivyo kufanya matokeo kuwa ya sare ya jumla ya 5-5.
Baada ya hapo timu hizo ziliingia tena uwanjani kwa dakika 30 za nyongeza ambazo dakika tano tu baadaye, Benzema alimaliza shughuli kwa mkwaju wa penalti ambayo ilitolewa baada ya mchezaji huyo kuchezewa rafu katika eneo la penalti.
Benzema alimpeleka kulia kipa wa City na mpira kujaa wavuni upande wa kushoto huku mashabiki wa City waliosafiri hadi jijini Madrid kushuhudia mtanange huo wakibaki vichwa chini wasiamini kilichotokea uwanjani hapo.
Matokeo hayo ni pigo jingine kubwa kwa kocha wa City, Pep Guardiola ambaye sasa anakuwa amepoteza mechi ya nusu fainali kwa mara ya sita huku akishindwa kuirudia rekodi yake ya mafanikio katika Ligi ya Mabingwa Ulaya aliyoiweka akiwa kocha wa Barcelona. Akiwa Barcelona kwa miaka minne, Pep aliweka rekodi ya kulibeba taji la ligi hiyo mara mbili.
Kimataifa Benzema aipeleka Real fainali Uefa
Benzema aipeleka Real fainali Uefa
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
