Madrid, Hispania
Unamzungumziaje kocha aliyewahi kuzinoa klabu za Juventus na AC Milan za Italia, kocha huyo huyo amezinoa Paris Saint-Germain ya Ufaransa, Chelsea ya England, Bayern Munich ya Ujerumani na Real Madrid ya Hispania.
Hapo unamzungumzia Carlo Ancelotti, kocha mwenye rekodi ya kuzinoa timu kubwa na maarufu katika nchi tano Ulaya, nchi zenye ligi kubwa zinazoongoza kuwa na mashabiki wengi wa soka duniani.
Katika ligi hizo, Ancelotti si tu amepita na kuondoka bali kote anajivunia kwa kuweka rekodi ya kuzipa mataji ya ligi zao yaani Serie A-Italia, Bundesliga-Ujerumani, EPL-England, Ligi 1-Ufaransa na La Liga kwa Hispania na hivyo kuwa kocha wa kwanza duniani kuchukua mataji katika ligi hizo kubwa duniani.
Ancelotti ambaye ni hivi karibuni ameipa Real Madrid taji la La Liga, pia ni kati ya makocha wenye rekodi ya kutwaa taji kubwa la klabu barani Ulaya au Ligi ya Mabingwa Ulaya ambalo amelichukua mara tatu mwaka 2013/14 akiwa Real Madrid na 2002/03 na 2006/07 akiwa AC Milan.
Hadi hapo Ancelotti anakuwa amemaliza kila kitu katika ngazi ya klabu, si tu amemaliza bali amemaliza akiwa ameweka rekodi katika nchi tano ambazo mashabiki wa soka kila siku wanataka kujua matokeo ya mechi za ligi hizo.
Kitu pekee ambacho hapana shaka kitamsumbua Ancelotti ni Kombe la Dunia, hakuwahi kulibeba taji hilo na kwa kuwa hajaonyesha dalili zozote za kutaka kustaafu, taji la dunia litakuwa katika fikra zake.
Binadamu ana kawaida ya kutorodhika, ni hivyo hivyo kwa Ancelotti, mataji yote aliyoyabeba huenda akayaona yanahitaji kuongezewa heshima ambayo ni kubeba taji la dunia.
Mpeleke Ancelotti Italia, mashabiki wa Milan wanakumbuka alivyowapa taji la Serie A, Chelsea anakumbukwa kwa taji la Ligi Kuu England au EPL, PSG kwa Ligi 1, Ujerumani-Bundesliga na Real Madri-La Liga, kote huko mashabiki wanamfahamu vizuri na sasa atahitaji dunia imfahamu kwa kutwaa taji la dunia. Tusubiri kwani hapana shaka kwamba hiyo ni moja ya shauku yake.
Kimataifa Ancelotti amebakisha Kombe la Dunia
Ancelotti amebakisha Kombe la Dunia
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
