Madrid, Hispania
Mwite kwa jina la wakala lakini Mino Raiola hana tofauti na dalali au mtu wa kati anayekutafutia chumba au nyumba Sinza jijini Dar es Salaam huku akipiga hesabu za kupata cha juu.
Tofauti yao ni kwamba Raiola anatambuliwa rasmi, ana leseni, analipa kodi na pesa anazopiga ni ndefu, lakini kimsingi wote kazi yao inakaribia kufanana, ni kazi ambayo haina presha, anatulia mahali tulivu, mguu juu, simu mkono wa kushoto, sigara mkono wa kulia, kinywaji pembeni, unakuja na yako anakutajia bei akiwa na uhakika wa kupata cha juu.
Hicho ndicho alichokuwa akikifanya Raiola kabla hajafariki dunia, akili yake saa zote ilikuwa ikiwaza ni vipi atapiga cha juu kwa kila mchezaji, hapo hesabu zake zilikuwa kwenye mamilioni ya dola, pauni au euro tofauti na madalali wengine tuliowazoea hapa Bongo licha ya kazi yao kufanana.
Raiola (54) aliyefariki Aprili 30 mwaka huu kwa maradhi ambayo hayakuwekwa wazi, angekuwa dalali Bongo angeambiwa ana kizizi anatumia uganga kwa namna ambavyo amekuwa akipiga pesa ndefu katika madili yake mengi ambayo yamehusisha wachezaji wa viwango vya juu duniani.
Hapo yumo nyota wa Manchester United, Paul Pogba ambaye licha ya kuwahi kuichezea timu hiyo huko nyuma lakini mwaka 2016, Raiola alifankisha mpango wa kumtoa Juventus na kumrudisha Old Trafford kwa ada iliyoweka rekodi ya Euro 120 milioni na kuwa mchezaji wa pili ghali duniani.
Katika orodha hiyo pia yumo, Erling Haaland aliyeanzia soka katika klabu ya Bryne FK ya kwao Norway na baadaye Molde FK lakini ni Raiola ambaye baadaye alifanikisha mpango wa kumuuza katika klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa ada ya Euro milioni 20.
Mwingine ni mshambuliaji mtukutu raia wa Sweden, Zlatan ibrahimovich ni Raiola aliyemtoa Juventus mwaka 2006 na kumuuza Inter Milan kwa ada ya euro milioni 10 na huo ukawa mwanzo wa safari za Zlatan katika klabu mbalimbali kuanzia Barcelona. AC Milan, PSG, Manchester United na LA Galaxy.
Marco Verratti naye ni mchezaji mwingine ambaye uwakilishi wa Raiola ulitumika, alianza kutamba nchini Italia na klabu ya Pescara kabla ya kuitwa timu ya Taifa, jicho la Raiola likamuona na hatimaye mwaka 2012, Raiola akafanikisha usajili wake katika klabu ya PSG kwa ada ya euro milioni 12.
Mwingine ni Matthijs De Ligt, Mholanzi aliyeanza kuonyesha uwezo wake katika klabu ya kwao Ajax, uwezo wake ulianza kuwavutia wengi na jicho la Raiola halikuwa mbali, kikafanyika kilichofanyika na hatimaye Julai, 2019, De Ligt akalazimika kuvaa jezi ya Juventus kwa ada euro milioni 75.
Raiola pia ndiye aliyehusika katika usajili wa Irving Lozano, mchezaji ambaye nyota yake ilianza kung’ara kwao Mexico akiwa na klabu ya Pachuca kabla ya kuelekea PSV Eindhoven ya Uholanzi na hapo hapo Raiola akapiga dili la uhakika lililomuwezesha Lozano kutua klabu ya Napoli ya Italia kwa ada ya euro milioni 42.
Hao ni baadhi tu ya wachezaji ambao Raiola amehusika kikamilifu katika usajili wao na kujiingizia fedha za maana kwani kila anapohusika katika mauzo ana mgao maana. Mfano unapozungumzia euro milioni 120 zilizotumika kwa Pogba, hapo unazungumzia fedha za Bongo kuanzia bilioni 200 na kuendelea.
Dalali anayefanya biashara ya fedha kiasi hicho si wa mchezo mchezo, hapo mgao wake ni wazi unacheza kwenye mamilioni, zungumzia milioni 100, 200 na kuendelea kutegemea na asilimia atakayolipwa na kumbuka huyo ni mchezaji mmoja tu hivyo tunaposema Raiola hakuwa dalali wa mchezo mchezo hiyo ndiyo maana yake.
Ipo hoja kwamba baadhi ya makocha hawawapendi watu kama Raiola kwa imani kwamba ndio wanaokuza thamani ya mchezaji na kuzifanya klabu ziingie gharama kubwa katika usajili kwa kutumia fedha ambazo wakati mwingine zingeweza kusajili mchezaji zaidi ya mmoja.
Kocha wa zamani wa Liverpool Rafa Benitez japo hakuwahi kukiri lakini aliwahi kuwa katika mgogoro na kiungo na nahodha wa timu hiyo, Steven Gerrard wakati mchezaji huyo alipokuwa akitaka kusaini mkataba mpya na klabu hiyo.
Gerrard amesimulia hilo katika kitabu cha historia ya maisha yake kwamba Benitez alitaka ajadiliane mkataba huo na mchezaji na si wakala au dalali jambo ambalo Gerrard alilikataa na kusisitiza kwamba wakala wake ndiye anayetakiwa kuhusika katika mazungumzo hayo.
Hoja ya Gerrard ilikuwa kwamba hata yeye Benitez alipokuwa akijadiliana mkataba wake na Liverpool alimtumia wakala wake hivyo haoni kwa nini naye asitumie wakala, suala hilo lilimalizwa kwa Gerrard kumtumia wakala wake kujadili mkataba mpya.
Kwa nini mawakala wanatumika, ipo hoja kwamba ndio wanaojua vyema thamani halisi ya mchezaji kuliko mchezaji mwenyewe, wana uwezo mkubwa wa kushawishi viongozi jambo ambalo wachezaji hawana, wanajua namna ya kufanya biashara kwa bei ya juu kuliko wachezaji, ni kama dalali anavyomshawishi mtu kupanga nyumba au chumba kwa bei ya juu, uwezo wa ambao mwenye nyumba hana au wakati mwingine hatambui thamani na uhitaji wa nyumba yake kwa watu wengine.
Kimataifa Mino Raiola;Dalali wa wanasoka aliyepiga pesa ndefu
Mino Raiola;Dalali wa wanasoka aliyepiga pesa ndefu
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
