na mwandishi wetu
Mechi ya mahasimu wa soka, Yanga na Simba imeisha kwa sare ya bila kufungana jioni hii huku habari mojawapo kubwa ikiwa ni mshambuliaji Fiston Mayele kukwama kuendeleza rekodi yake ya mabao au kutetema katika Ligi Kuu ya NBC Bara.
Mayele ambaye ni kinara wa mabao katika ligi hiyo akiwa na mabao 12, amekuwa na rekodi nzuri ya mabao mfululizo katika mechi sita zilizopita na ilitarajiwa aipendezeshe rekodi hiyo kwa kuiendeleza katika mechi hiyo kubwa Afrika Mashariki iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Kushindwa huko kwa Mayele kupachika mabao na hatimaye kutetema kwa kiasi kikubwa kumechangiwa na mabeki wawili wa Simba, Joash Onyango na Enock Inonga ambao walijipanga vyema katika kuhakikisha mchezaji haleti madhara langoni mwao.
Katika mechi ya mzunguko wa kwanza ya mahasimu hao ambayo pia iliisha kwa matokeo ya sare ya bila kufungana, walikuwa ni Inonga na Onyango pia ambao walimuweka kwapani Mayele ambaye alijikuta akienda benchi katika dakika ya 83.
Safari hii Inonga na Onyango walionekana kujipanga vizuri zaidi kwa kupokezana majukumu jambo ambalo lilifanikiwa.
Kasi ya Mayele kusaka bao ilionekana mapema katika dakika ya 11, alipoifumania pasi ndefu lakini wakati akitaka kupiga shuti Onyango alikuwa karibu na kumdhibiti.
Dakika tatu baadaye, Mayele aliunganishiwa pande na Djuma Shaban lakini wakati akielekea kumkabili kipa wa Simba Aishi Manula, Inonga alilala chini na kuuwahi mpira. Baada ya kuuwahi mpira huo, Inonga akiwa mwenye furaha aliinua mkono juu kama ishara ya kudhihirisha jinsi alivyomdhibiti Mayele.
Wawili hao walikutana tena dakika ya 23 kuwania pasi iliyotokea upande wa kulia lakini alikuwa ni Inonga kwa mara nyingine aliyeuwahi mpira na kumuacha Mayele akiwa hana la kufanya.
Dakika ya 32 tena Mayele alidhibitiwa na safari hii ilikuwa zamu ya Onyango ambaye alilala chini kuuwahi mpira na kuutoa nje wakiwa wanauwania na Mayele huku Onyango akionekana kuchoshwa na tukio hilo.
Dakika ya 56 tena Mayele aliunganishiwa pasi na akiwa katika mbio za kuelekea kwa Manula, Inonga kwa mara nyingine alilala chini na kuuwahi vizuri mpira.
Wakati mashabiki wakiwa wamekata tamaa dakika za lala salama, Mayele nusura aipatie Yanga bao alipoinasa pasi ndefu ya juu lakini shuti lake lilienda kwenye nyavu za pembeni, hivyo hivyo kwa Simba, Mugalu aliupigia vizuri hesabu mpira wa juu na kuufuata hewani kabla ya kuupiga kichwa lakini kipa Diarra alikuwa karibu na kuudaka.
Nje ya matukio hayo, mechi hiyo pia ilitawaliwa na ubabe na tafrani za hapa na pale hali iliyomfanya mwamuzi Kayoko wakati mwingine kuweka kando filimbi yake na kuingilia kati katika kuwasuluhisha wachezaji hao.
Hali hiyo ilianza kujitokeza katika dakika ya 26, Morison na kipa wa Yanga Diarra nusura wachapane makonde kabla ya kudhibitiwa na wachezaji wenzao akiwamo mwamuzi ambaye juhudi zake za kuwasuluhisha zilionekana hasa katika kumdhibiti Morisson lakini baadaye aliwapa wachezaji hao kadi ya njano kila mmoja.
Tafrani ya pili ilitokea kati ya Aucho na Mugalu ambao nao nusura washikane lakini pia ikatokea tafrani nyingine kati ya Inonga na Moloko ambapo, Inonga alipewa kadi ya njano licha ya mchezaji huyo kuonekana akimshika begani Moloko ikiwa ni ishara ya kumaliza ugomvi. Wakati wote wa tafrani hiyo, Kayoko hakuishia kutumia filimbi tu bali hata mikono yake kusuluhisha.
Kwa sare hiyo, Yanga inaendelea kujiimarisha kileleni ikiwa na pointi 55 wakati Simba inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 42. Timu hizo huenda zikakutana tena katika mechi ya Kombe la FA iwapo Simba itaibuka kinara mbele ya Pamba.
Soka Mayele ashindwa kutetema
Mayele ashindwa kutetema
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
