Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imesema haina cha kuuthibitishia umma na mashabiki juu
ya uwezo wao msimu huu, isipokuwa Simba ndio watakaokuwa na mtihani
mkubwa katika mechi dhidi yao Jumamosi hii.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Yanga, Hassan Bumbuli
amebainisha kuwa wapinzani wao hao ndio wanaohitaji kuwafuta machozi
mashabiki wao baada ya kutolewa kwenye robo fainali ya Kombe la
Shirikisho Afrika na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Bumbuli aliongeza kuwa Simba pia wanahitaji kuonesha kuwa wako vizuri
kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara zaidi ya Yanga kupitia mechi hiyo
kitu ambacho anaamini kitawawia vigumu kwa kuwa wao pia wanahitaji
ushindi ili kuongeza pengo la pointi kileleni mwa msimamo wa ligi.
Timu hizo zitaingia kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Yanga ikiwa
kileleni kwa pointi 54 dhidi ya Simba yenye pointi 37 inayoshika
nafasi ya pili.
“Sisi mipango yetu inakwenda vizuri, timu ipo kambini inajiandaa na
mchezo huo, tunaamini utakuwa mchezo mzuri, hatuangalii kama wao
wamejeruhiwa au wamefanywa nini, sisi tunaangalia kama watakuja
tutawakaribisha kwenye ligi ambayo ina mfalme wake,” alisema.
“Tunawakaribisha kwenye mechi ya kwanza wamerudi wakiwa mikono mitupu
halafu wanakuja kukutana na mwamba kileleni hajapoteza mchezo, wao
wana kazi kubwa ya kuthibitisha kwa watu wao, sisi tumethibitisha
mengi kwa watu wetu kuanzia njia ya ubingwa msimu huu na hata
tukipoteza bado hatuna tatizo kulingana na ukubwa wa pointi
tulizonazo,” alisema Bumbuli.
Simba ambayo inapambana kutetea ubingwa wake wa tano mfululizo msimu
huu, pia ipo robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam ikisubiri
kupepetana na Pamba na ikifanikiwa kupenya hapo itakutana na Yanga
kwenye hatua ya nusu fainali.
Yanga yenyewe ilifika hatua hiyo baada ya kuifunga Geita Gold kwa
mikwaju ya penalti 7-6 baada ya dakika 90 za mchezo huo kuisha kwa
sare ya bao 1-1.
Soka Bumbuli: Uwezo wetu unajulikana, kazi wanayo Simba
Bumbuli: Uwezo wetu unajulikana, kazi wanayo Simba
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
