Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ameeleza kuwa licha ya kumkosa kiungo mshambuliaji wake, Saido Ntibazonkiza, anaamini ana kikosi kipana kitakachompa matokeo keshokutwa Jumamosi.
Simba ambayo inatarajiwa kuwasili mjini Conakry, Guinea leo usiku kwa ajili ya mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya AC, imeondoka na wachezaji 24 akikosekana nyota huyo aliyesajiliwa hivi karibuni.
Wengine waliokosekana kwenye safari hiyo ni Jonas Mkude, Peter Banda na Jimmyson Mwanuke huku ikielezwa Saido ameshindwa kuambatana na timu kwa kuwa ni majeruhi.
Robertinho alisema kuwa Saido ni mchezaji muhimu ndani ya kikosi hicho hawezi kulikataa hilo lakini anashukuru kuona Simba ina kikosi kipana na wapo wachezaji watakaomudu kuziba nafasi yake.
“Kwenye soka huwezi kupata unachohitaji kila wakati, nafahamu Saido ni mchezaji muhimu lakini nashukuru kuona wapo wengine wazuri ndani ya kikosi, nitawatumia na ninaamini watafanya vizuri kwenye eneo la kiungo.,” alisema Robertinho.
“Lengo tulilonalo ni kupata ushindi na kucheza vizuri tukiwa na mikakati mizuri, kukaba kwa juhudi eneo la kiungo, kuongeza nafasi katikati ya njia hivyo tunafikiria ushindi na tunafikiria makubwa,” alisema.
“Tumepita kufika hapa na sasa tunafikiria ubingwa,” alisema jana Robertinho timu hiyo ilipotua Addis Ababa, Ethiopia kabla ya kuunganisha safari ya kuelekea Conakry iliyoanza leo majira ya saa tano asubuhi.
Alisema anaamini kwenye kupambana na kwenye mbinu na zaidi kwenye maeneo hayo wamejizatiti kuhakikisha wanapata matokeo na kusonga mbele kwenye hatua hiyo na lengo likiwa kutwaa ubingwa.
Simba iliyoanza safari yake leo alfajiri, inatarajia kucheza mechi yake hiyo Jumamosi saa 1.00 jioni kwenye Uwanja wa Jenerali Conte, Conakry.
Wekundu hao wakimalizana na Horoya ambao ni mabingwa mara nane mfululizo wa Ligi Kuu ya Guinea, watapapatuana na Raja Casablanca ya Morocco wakiwa nyumbani Februari 18 kabla ya kukipiga na Vipers ya Uganda Februari 25, mwaka huu wakiwa ugenini.
