Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Azam FC, Dani Cadena ameahidi kuifunga Simba ili kurudisha furaha kwa mashabiki wao baada ya kupoteza matumaini yao ya ubingwa wa Ligi Kuu NBC msimu huu.
Timu hizo zinatarajia kuumana Febuari 21, mwaka huu ukiwa ndio mchezo unaofuata baina ya timu hizo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Kwenye mechi ya awali msimu huu, Azam iliifunga Simba bao 1-0.
Kocha huyo raia wa Hispania alisema pamoja na kupoteza matumaini ya ubingwa lakini wanataka kumaliza ligi nafasi tatu za juu na hilo linawezekana endapo watashinda mechi zao zijazo ikiwemo dhidi ya Simba.
“Tunajua utakuwa mchezo mgumu kwetu kwa kuwa Simba ipo kwenye mbio za ubingwa lakini nasi hatupo tayari kuona tunaendelea kupoteza sababu tupo katika vita kubwa ya kumaliza nafasi ya tatu dhidi ya Singida Big Stars,” alisema Cadena.
Kocha huyo ameeleza kuwa anajua Simba watakuja kwa nguvu kutaka kulipa kisasi baada ya kuwafunga bao 1-0 kwenye mzunguko wa kwanza lakini kikosi chake kimejipanga kuhakikisha kinafanya vizuri.
Alisema mapumziko waliyonayo tangu baada ya mchezo wao wa mwisho dhidi ya Dodoma Jiji ambapo walipoteza kwa mabao 2-1 yamezidi kuwaimarisha na ndio maana anaamini watafanya vizuri kwenye mechi nane zilizosalia kabla msimu kumalizika.
Azam ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 43 sawa na Singida BS iliyo nafasi ya nne, lakini Azam ina wastani mzuri wa mabao ya kufunga.
