Benfica, Ureno
Hatimaye klabu ya Chelsea imefanikiwa kumsajili kiungo Enzo Fernandez kutoka klabu ya Benfica ya Ureno kwa ada ya Pauni 131 milioni na mkataba wa miaka minane na nusu. Benfica imethibitisha.
Taarifa ya klabu ya Benfica iliyopatikana jana Jumanne jioni ilithibitisha makubaliano baina ya timu hizo kuhusu namna Chelsea watakavyolipa ada ya uhamisho kwa kiungo huyo wa Argentina mwenye umri wa miaka 22.
Uhamisho wa Enzo unakuwa umeweka rekodi katika Ligi Kuu England ukiipiku rekodi ya Manchester City ambao mwaka 2021 walilipa Pauni 100 milioni kumsajili Jack Grealish kutoka Aston Villa.
Chelsea inasubiriwa kuthibitisha usajili huo ingawa taarifa za England zinadai kuwa klabu hiyo imefuata taratibu zote za kimaandishi na kuziwasilisha kwa wakati kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa jana Jumanne saa tano usiku.
Enzo alikuwa mmoja wa wachezaji nyota walioibeba timu ya Taifa ya Argentina kwenye fainali za Kombe la Dunia akitwaa tuzo ya mwanasoka bora wa umri mdogo wakati Argentina ikibeba Kombe la Dunia kwa kuilaza Ufarana kwa penalti 4-2 baada ya sare ya mabao 3-3 katika dakika 120.
Habari zaidi zinadai kwamba mchezaji huyo tayari alishakubaliana mambo kadhaa binafsi na klabu ya Chelsea na ndiye aliyekuwa akiihimiza Benfica kukamilisha usajili huo.
Enzo anakuwa mchezaji wa saba kusajiliwa Chelsea akiwa ametanguliwa na David Datro Fofana, Malo Gusto, Andrey Santos, Benoit Badiashile, Mykhailo Mudryk na Noni Madueke.
Kukamilika kwa usajili wa mchezaji huyo hakujamfurahisha kocha wa Benfica, Roger Schmidt ambaye hakupenda mchezaji huyo aondoke na alichukizwa kwa namna Chelsea ilivyoendesha mikakati ya usajili huyo.
Kimataifa Hatimaye Chelsea yamnasa Enzo
Hatimaye Chelsea yamnasa Enzo
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
