Na mwandishi wetu
Timu ya Simba kesho inashuka dimbani kuvaana na Coastal Union huku ikieleza tahadhari iliyonayo juu ya mchezo huo wa hatua ya 32 bora ya Kombe la FA (ASFC), utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Simba imeeleza kuwa pamoja na kuwa kwenye uwanja wa nyumbani katika mchezo huo lakini wanauchukulia tofauti kwa ukubwa na uzuri wa wapinzani wanaokutana nao.
Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally ameeleza kuwa wanashukuru wanaingia katika mchezo huo wakiwa kamili na maandalizi ya kutosha lakini wanauheshimu uwezo wa Coastal na upambanaji wao hivyo wataingia dimbani kwa tahadhari.
“Coastal ni timu nzuri na kubwa na ukiangalia siyo timu ya kubeza, hivyo tumejiandaa na kujiandaa na tuna tahadhari juu yao maana tunakwenda kucheza na timu ambayo msimu uliopita iliingia fainali ya michuano hii.” Alisema Ally.
“Kwa hiyo tunafahamu ugumu uliopo ndiyo maana tumekuwa kwenye maandalizi kabambe ya kuhakikisha tunatafuta matokeo yatakayotupeleka mbele katika mchezo huu,” alisema Ally.
Naye kocha msaidizi wa Coastal, Yusuf Lazaro ameeleza kuwa kamili kwa ajili ya mechi hiyo wakihitaji kufanya vizuri kwa mara nyingine licha ya kufahamu uzuri wa timu ya Simba kwa sasa.
“Hakuna asiyefahamu Simba wako vizuri kwa sasa na sisi tunalitambua hilo ndiyo maana tumejipanga na kujiandaa kwa ajili ya mechi hiyo ambayo haitakuwa nyepesi lakini tumedhamiria kupambania ushindi na kutafuta tiketi ya kusonga mbele zaidi,” alisema Lazaro.
Simba ilitinga hatua hiyo baada ya kuifurumusha Eagle FC kwa mabao 8-0 wakati Coastal waliofungwa kwa penalti 4-1 na Yanga kwenye fainali iliyopita ya michuano hiyo baada ya sare ya 3-3 ya dakika 90 za kawaida, yenyewe katika hatua iliyopita ilifanikiwa kuifunga Tanga Middle mabao 3-1.
Mechi nyingine ya michuano hiyo inatarajiwa kupigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ikizikutanisha KMC na Copco FC.
