Na mwandishi wetu
Timu ya Coastal Union imeendelea kujiimarisha baada ya kukamilisha usajili wa winga Juma Mahadhi kutoka Geita Gold ya mkoani Geita.
Katibu Mkuu wa Coastal Union, Omari Ayoub ameeleza kuwa hiyo ni katika mipango ya kukiboresha kikosi chao ili kifanye vizuri kwenye mechi zilizosalia za Ligi Kuu NBC pamoja na Kombe la FA.
“Ni kweli tumemrudisha nyumbani Mahadhi kutoka Geita FC, lakini pia tupo kwenye hatua za mwisho kukamilisha usajili wa beki wa kimataifa kutoka Jamhuri ya Demokrasi ya Congo, Felly Mulumba, naamini hadi kufikia siku ya mwisho kila kitu kitakuwa tayari,” alisema Ayoub.
Kiongozi huyo ameeleza kuwa usajili huo umetokana na mapendekezo ya benchi lao la ufundi ambalo linaongozwa na kocha Joseph Lazaro na mkurugenzi wa ufundi, Bakari Shime.
Kiongozi huyo ameeleza kuwa nafasi waliyopo kwenye msimamo siyo nzuri hivyo kwa usajili huo, imani yao ni kwamba watarudi kwenye mwenendo mzuri wa kupata matokeo mazuri na kujiondoa katika nafasi mbaya waliyopo sasa.
Coastal ipo nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi, ikikusanya pointi 17 katika michezo 19 ambayo wamecheza msimu huu.
Soka Mahadhi atua Coastal Union
Mahadhi atua Coastal Union
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
