London, England
Hatimaye klabu ya Chelsea imefanikiwa kumsajili kwa mkopo mshambuliaji wa Atletico Madrid, Joao Felix hadi mwisho wa msimu huu kwa ada inayotajwa kufikia Pauni 9.7 milioni.
Sambamba na hilo, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ureno mwenye umri wa miaka 23 pia amesaini kuongeza mwaka mmoja katika mkataba wake na Atletico ambao sasa utafikia ukomo Juni 2027.
Akizungumzia usajili huo, kocha wa Chelsea, Graham Potter amesema janga la kuwa na wachezaji wengi majeruhi limeifanya timu hiyo kuongeza nguvu katika kuisaka saini ya mchezaji huyo huku Christian Pulisic naye akitarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa miezi kadhaa.
“Ni mchezaji wa kiwango, ataleta utofauti hapa na najiandaa kufanya naye kazi, bado kijana lakini ana uzoefu mkubwa na hilo linatupa msaada,” alisema Potter.
“Nimekuwa makini na baadhi ya wachezaji wazuri kwa muda mrefu lakini tatizo la kuwa na majeruhi labda ndilo lililotufanya tuharakishe, lakini ni jambo zuri kuwa naye na amefanya mazoezi leo (jana Jumatano) jambo ambalo ni zuri,” alisema Potter.
Felix mbali na Chelsea pia alikuwa akiwaniwa na Arsenal na Man United lakini ni Chelsea waliokuwa mstari wa mbele na hatimaye wamekamilisha usajili huo na moja kwa moja wanakuwa na jukumu la kumlipa mshahara wote kwa kipindi kilichobaki msimu huu ikiwa ni sehemu ya mkataba huo.
“Chelsea ni moja ya timu kubwa duniani, natarajia kuisaidia timu kufikia malengo yake, nina furaha sana kuwa hapa na inafurahisha kucheza Stamford Bridge,” alisema Felix.
Felix alikuwa kwenye kikosi cha Ureno kilichoshiriki fainali za Kombe la Dunia na kuishia hatua ya robo fainali akifunga bao moja katika mechi tano.
