Paris, Ufaransa
Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Ufaransa (FFF) imemtaka rais wa shirikisho hilo, Noel le Graet kujiuzulu kutokana na kauli alizozitoa kuhusu mwanasoka wa zamani wa Ufaransa, Zinedine Zidane.
Le Graet (pichani juu) alijikuta akishutumiwa baada ya kusema kwamba asingekuwa tayari japo kupokea simu ya Zidane wakati mchezaji huyo wa zamani akihusishwa na mipango ya kuinoa timu ya Taifa ya Ufaransa.
Na ingawa baadaye Le Graet aliomba radhi, Kamati ya Maadili ya FFF ikiongozwa na Patrick Anton imedai kwamba ni wakati sahihi kwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 81 kukaa pembeni.
Akizungumza na jarida moja la Ufaransa, Anton alisema,
“Le Graet ametoa kauli ambayo inaonyesha kwamba kidogo amepoteza uelewa aliokuwa nao, ni mtu ambaye amechoka na anahitaji kuendelea na mambo mengine.”
Zidane au Zizou aliisaidia Ufaransa kubeba Kombe la Dunia mwaka 1998 akiwa mchezaji na akiwa kocha wa Real Madrid ameiwezesha timu hiyo kubeba mataji kadhaa likiwamo taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya zaidi ya mara moja.
Katika siku za karibuni Zizou alikuwa akitajwa kumrithi kocha wa Ufaransa, Didier Deschamp baada ya timu hiyo kushindwa na Argentina katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia lakini mpango huo ulikwama baada ya Deschamps kuongeza mkataba na ataendelea kuinoa timu hiyo hadi mwaka 2026.
Kauli ya Le Graet imekuwa ikitajwa na wengi kuwa ni ya kumkosea heshima mchezaji huyo wa zamani huku kipa wa Ufaransa aliyestaafu kuichezea timu hiyo, Hugo Lloris na mshambuliaji Kylian Mbappe nao wakimshutumu bosi huyo wa FFF.
