Milan, Italia
Mwanasoka nyota wa zamani wa klabu za Chelsea na Juventus, Gianluca Vialli amefariki dunia akiwa na miaka 58 kwa maradhi ya saratani baada ya kuugua maradhi hayo kwa miaka mitano sasa.
Vialli amefariki dunia siku tatu baada ya kuzikwa kwa Mfalme wa soka, Pele ambaye alizikwa Jumanne iliyopita baada ya kufariki dunia usiku wa Desemba 29 kwa maradhi ya saratani akiwa na 82.
Vialli ambaye ni Mtaliano, kwa mara ya kwanza alibainika kuwa na maradhi ya saratani au kansa mwaka 2017 na mwaka 2021 vipimo vikaonyesha kwamba tatizo linazidi kuwa kubwa.
Taarifa ya familia ya mchezaji huyo iliyopatikana leo Ijumaa ilieleza, “Akiwa amezungukwa na wanafamilia wake, akafariki dunia usiku ni baada ya kuugua kwa miaka mitano, alionyesha ujasiri na uvumilivu.”
“Tunawashukuru wote ambao walikuwa wakimuunga mkono kwa miaka yote aliyokuwa akisumbuliwa na maradhi kwa namna walivyoguswa na tatizo lake, kumbukumbu na mifano yake ya kuigwa itaendelea kuishi katika mioyo yetu kwa maisha yote,” ilifafanua taarifa hiyo.
Vialli alikuwamo katika jopo la makocha walioiongoza Italia kwenye fainali za Euro 2020 kwa mafanikio lakini aliamua kujiondoa kwenye kazi hiyo Desemba ili apate nafasi ya kushiriki katika matibabu ya maradhi ya saratani yaliyokuwa yakimsumbua.
“Najua huenda nisife kwa umri mkubwa, natumaini kuishi kwa muda mrefu kadri iwezekanavyo lakini najiona dhaifu zaidi kuliko ilivyokuwa awali,” alisema Vialli kupitia makala ya Netflix ambayo ilirushwa Machi 2022.
Aliutaja ugonjwa wa saratani kama ni mwenza katika safari yake, mwenza ambaye aliamini hatimaye utafika wakati atamuacha akiwa kwenye amani baada ya kuujaribu ujasiri wake. “Maradhi yanaweza kukufunza mengi kuhusu wewe ni nani na kutufanya tujiweke katika mtazamo tofauti na jinsi tunavyoishi,” alisema Vialli.
Baada ya taarifa za kifo hicho kutolewa, Rais wa Shirikisho la Soka Italia, Gabriele Gravina alisema, “Gianluca alikuwa mtu muungwana na aliishi katika namna nzuri katika timu ya Taifa na kwa wote ambao walivutiwa na sifa zake za kibinadamu zisizo za kawaida.”
Mbali na Juventus na Chelsea ambapo pia aliwahi kuwa kocha mchezaji, Vialli pia amewahi kuichezea klabu ya Sampdoria ya Italia. Ameacha mke na watoto wawili wa kike.
