Na mwandishi wetu
Kocha Msaidizi wa Simba, Juma Mgunda amekubali matokeo baada ya kutolewa kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayoendelea visiwani Zanzibar huku akisema mwaka huu haikuwa bahati yao.
Simba jana iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KVZ lakini ushindi huo haukuisaidia miamba hiyo ya Tanzania Bara kusonga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo kutokana na kuzidiwa kwa pointi na Mlandege FC iliyomaliza vinara kwenye Kundi C.
Mgunda ameeleza kuwa pamoja na kutolewa kwenye hatua ya makundi lakini kuna vitu ambavyo wamefaidika navyo ikiwemo kuona uwezo wa baadhi ya wachezaji ambao hawatumiki mara kwa mara kwenye mechi za Ligi Kuu NBC.
“Tumetolewa kwenye mashindano lakini kuna mazuri na mapungufu tumeyaona na uzuri kocha mkuu (Robert Oliveira) yupo naye ameyaona, kitu cha msingi tutakwenda kuyafanyia kazi mapungufu ili wachezaji wetu wote wawe kwenye viwango vinavyofanana.
“Kitu kizuri kilichonifurahisha ni vile vitu ambavyo watu wengi walikuwa wanalalamika wachezaji hawapati nafasi, kupitia mashindano haya wamewaona na mpira ni mchezo wa wazi naamini hawatokuwa na maswali tena,” alisema Mgunda.
Hata hivyo, tayari timu hiyo imerejea jijini Dar es Salaam leo mchana kwa ajili ya kuendelea na mandalizi ya mashindano yaliyopo mbele yao ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu ikionekana ni kitu kizuri kurejea kwao mapema kwani watakuwa na muda mzuri wa kujipanga kabla ya kuanza kwa mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa.
Bado haijawekwa wazi, Wekundu hao watajichimbia wapi kwa ajili ya maandalizi yao hayo lakini Kocha Mkuu, Oliveira wakati anatambulishwa hivi karibuni, uongozi ulisema endapo wangetolewa basi watatafuta kambi Tanzania au nje ya nchi kwa ajili ya kujiandaa na michuano mikubwa inayowakabili.
