Na mwandishi wetu
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemuita kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ kujadili hatma ya mkataba wake na Yanga SC.
Shirikisho hilo limefikia hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko ya Yanga kuhusiana na mchezaji huyo kutangaza kuvunja mkataba wake na timu hiyo tangu Desemba 22, mwaka jana, mkataba unaotajwa kufika ukomo Mei, 30 mwaka 2024.
Kwa mujibu wa barua ya TFF, Fei anatakiwa kwenda na mshauri wake wa kisheria mbele ya kamati hiyo kesho Jumatano kwenye Ofisi za TFF, Uwanja wa Karume, Dar es Salaam kwa ajili ya kusikiliza malalamiko hayo.
“Kwa barua hii, unaitwa kufika na mshauri wako wa kisheria mbele ya kamati siku ya Jumatano, tarehe 4 Januari 2023 katika Ofisi ya TFF, Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kwa ajili ya kusikiliza malalamiko hayo,” ilieleza sahemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo, taarifa nyingine zinafafanua kuwa kikao hicho kina uwezekano wa kusikilizwa keshokutwa, Ijumaa baada ya Fei kurejea akitokea Falme za Kiarabu anakotajwa kuwa yupo huko kwa sasa.
Fei alivunja mkataba huo akiutolea ufafanuzi wa vipengele vya kimkataba vilivyompelekea kufanya hivyo pamoja na kurejesha fungu la usajili la Sh 112,000,000 ambalo baadaye lilirejeshwa na Yanga ambao walieleza msimamo wao wa kutokukubaliana na suala la kuvunjwa kwa mkataba wa mchezaji huyo na klabu hiyo.
Yanga ilifafanua kuwa mchezaji huyo bado ni halali yao kwa mujibu wa mkataba na kwamba ilishaanza maongezi juu ya kumuongeza mkataba mwingine licha ya kuwa alibakiza miaka miwili ya mkataba aliousaini mwaka 2020.
Awali, siku chache baada ya vuguvugu hilo, duru mbalimbali za michezo zilieleza kuwa kiungo huyo anakwenda Azam FC kabla ya Mtendaji Mkuu wake, Abdulkarim Amin ‘Popat’ kukanusha taarifa hizo akidai kuwa klabu yao haihusiki na lolote.
Soka Kamati TFF yamuita Fei Toto
Kamati TFF yamuita Fei Toto
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
