Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Polisi Tanzania, Mwinyi Zahera amesema sare waliyoipata kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union imewapa matumaini ya kushinda mchezo ujao dhidi ya Ruvu Shooting, timu ambayo imekosa matokeo mazuri katika mechi za hivi karibuni.
Zahera amesema kuwa matumaini aliyonayo na mabadiliko ya ndani ya kikosi ni kutokana na wachezaji wake kushika vyema mbinu na maelekezo anayowapa kwenye uwanja wa mazoezi.
“Tunacheza na Ruvu Shooting ni timu nzuri licha ya kutokuwa na matokeo mazuri lakini Polisi hii siyo ile ya siku za nyuma, timu imeimarika kwa kiasi kikubwa naamini mwaka mpya tutauanza vizuri na watu watashangaa kuona matokeo yakibadilika na kupanda nafasi za juu,” alisema Zahera.
Zahera ameeleza kuwa pamoja na timu yake kuwa mkiani mwa msimamo wa ligi lakini hawawezi kushuka daraja kutokana na mikakati waliyonayo na maboresho wanayotarajia kuyafanya kwenye dirisha hili dogo la usajili.
Zahera alisema anajua mechi zilizobaki ni ngumu na ligi ina ushindani mkubwa lakini endapo atafanikiwa kupata wachezaji anaowataka kwenye dirisha dogo anaamini timu hiyo itasalia kushiriki ligi kuu ya msimu ujao.
Polisi imeshinda mechi mbili pekee, sare mechi nne na kupoteza michezo 12, kitu ambacho kinawafanya kubaki nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 10.
