Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda, amewataka wachezaji wake kucheza kwa umakini wa hali ya juu mechi zao za Ligi Kuu NBC zilizosalia ili kuhakikisha wanashinda na kupunguza pengo la pointi kati yao na vinara wa ligi, Yanga SC.
Simba ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa imekusanya jumla ya pointi 41 huku watani zao Yanga wakiwa kileleni kwa kukusanya pointi 47 baada ya timu zote kushuka dimbani mara 18.
Mgunda ameeleza kwa namna ushindani ulivyo hivi sasa hawapaswi kuidharau timu yoyote kwenye ligi na hiyo ni kutokana na malengo waliyokuwa nayo msimu huu ya kurudisha mataji yao yote likiwemo la Ligi Kuu lililotua Yanga msimu uliopita.
“Niseme ukweli ushindani uliopo kwenye mbio za ubingwa kwa sasa ni mkubwa, ukipoteza au kutoka sare mchezo mmoja umetoa nafasi kubwa sana kwa mpinzani wako, ukiangalia pengo la pointi sita kati yetu na Yanga ni kubwa hivyo lazima wachezaji waongeze umakini kuhakikisha tunashinda ili kupunguza hilo,” alisema Mgunda.
Kocha huyo alikiri kuwa kitendo cha wapinzani wao Yanga kuendelea kushinda mechi zao za ligi kinawapa hofu kwani kinafifisha matumaini yao ya kuwaondoa kileleni huku mbaya zaidi ligi yenyewe ikiwa ipo kwenye mzunguko wa mwisho.
Mgunda pia amezungumzia usajili wa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Saido Ntibazonkiza kuwa utaongeza kitu kwenye kikosi chake kutokana na uzoefu aliokuwa nao mchezaji huyo ambaye amecheza soka la kulipwa hadi barani Ulaya.
Alisema mbali na mkongwe huyo, kwa ujumla anafurahishwa na upambanaji wa wachezaji wake wote katika kupigania mafanikio ya timu hiyo hasa katika kipindi hiki ambacho nguvu zao wamezielekeza kwenye kubeba ubingwa wa Ligi Kuu.
Keshokutwa Ijumaa kikosi cha Simba kitaikabili Tanzania Prisons, huo ukiwa mchezo wa raundi ya 19 kwenye ligi na ni wa mwisho kwa mwaka 2022 baada ya hapo timu hiyo itaelekea visiwani Zanzibar kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi.
