Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema kuwa kutuliza akili, kufuata maelekezo na kurudi mchezoni kumewasaidia kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya KMC jana Jumatatu.
Simba ilipata ushindi huo kwenye mechi iliyopigwa jana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ambapo mpaka dakika ya 52 matokeo yalikuwa bao 1-1 kabla ya Simba kucharuka na kumaliza mechi kwa ushindi huo mnono.
Mgunda alisema wanashukuru wamepata pointi tatu muhimu dhidi ya KMC ambao walikuwa wakicheza nao kwa uangalifu mkubwa kutokana na ubora wao wa kucheza kitimu lakini wachezaji wake walifahamu nini cha kufanya na kupata matokeo.
“Pamoja na yote kwenye mpira lolote linatokea, baada ya wao kusawazisha ilibidi turudi mchezoni, turudi kwenye malengo na mipango yetu, tutulize akili na mwisho niwashukuru wachezaji kwa kazi nzuri waliyofanya kwa kucheza jinsi ambavyo tumeelekezana na kushinda mechi.
“Lakini kingine kikubwa kwa sasa tunajitahidi sana kufanya mazoezi ya kufunga mabao maana ili ushinde ni lazima ufunge kwa hiyo tunajitajidi mazoezi hayo ili tupate mabao na ndiyo maana sasa kumekuwa na mchanganyiko wa wafungaji,” alisema Mgunda.
Kocha wa KMC, Hitimana Thierry aliwapongeza Simba kwa kutumia vizuri nafasi walizozipata lakini alieleza kutoridhishwa na maamuzi ya mwamuzi wa mchezo huo akidai hawakutendewa haki sehemu kadhaa na kuwakandamiza.
“Nafikiri Simba walikuwa bora kwenye kutumia nafasi, kila nafasi waliyopata walifunga, ukizungumza 3-1 ni mazungumzo lakini ukifuata mechi ilivyo mwamuzi hakuwa vizuri kiukweli, hakututendea haki, timu kubwa ni kubwa lakini waamuzi wachezeshe haki japo tunakubali matokeo na tunawapa hongera Simba,” alisema Hitimana.
Kwa ushindi huo Simba sasa imefikisha mabao 40 ya kufunga msimu huu ambayo ni mengi zaidi ya timu yoyote ingawa imeendelea kusalia nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi Kuu NBC ikiwa na pointi 41 huku KMC ikishika namba tisa kwa pointi 22 baada ya mechi 18.
Soka Mgunda ataja siri ya mabao matatu
Mgunda ataja siri ya mabao matatu
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
