Na mwandishi wetu
Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amesema ushindi wa mabao 3-0 walioupata katika mechi dhidi ya Coastal Union umekuja baada ya kuingia uwanjani kwa tahadhari kwa kuwa waliufahamu ubora wa wapinzani wao.
Yanga jana Jumanne iliumana na Coastal katika mechi ya Ligi Kuu NBC na kuibuka na ushindi huo ikifaidika na mabao yaliyofungwa na Fiston Mayele aliyeingia nyavuni mara mbili na Feisal Salum au Fei Toto akihitimisha ushindi kwa kuandika bao la tatu.
Kaze alisema kuwa walijua hauwezi kuwa mchezo rahisi kwani Coastal ni timu yenye wachezaji bora kwenye safu ya ushambuliaji na wana wachezaji wazuri hivyo waliingia kwa tahadhari kubwa na mwisho imewasaidia wamepata matokeo ya ushindi mnono.
“Tulijua kuwa ili tufunge tunapaswa kuwa na subira, tucheze kwanza mpira wao wacheze nyuma ya mpira, watachoka halafu tutapata njia za kufunga mabao.
“Kipindi cha kwanza hatukupata nafasi nyingi, kipindi cha pili walichoka baada ya kukimbia nyuma ya mpira tukapata mabao mawili, kikubwa ilikuwa mechi nzuri kutokana na umakini waliouonyesha na kutusaidia kimaandalizi kuelekea mechi zijazo,” alisema Kaze.
Alisema kila mechi wanayoenda kucheza wanazingatia walichokifanya katika michezo iliyopita na mechi inayofuata, hivyo imewasaidia kuwajenga ukizingatia mechi yao inayofuata dhidi ya Azam inayotarajiwa kupigwa Jumapili hii.
Naye Kocha msaidizi wa Coastal Union, Joseph Lazaro, alisema kwamba ulikuwa mchezo mgumu, waliingia kwa ajili ya kutafuta pointi tatu lakini ubora wa Yanga umeamua mechi hiyo.
“Tuko kwenye kipindi kigumu, tumeondokewa na kocha mkuu (Yusuf Chipo) tukiwa kwenye maandalizi hivyo kuna vitu havikwenda tulivyopanga japo nawapongeza Yanga kwa ushindi walioupata ingawa wachezaji wangu walipambana na bahati haikuwa yetu.
“Hatujafanya vizuri kwenye michezo zaidi ya nane mfululizo, sasa tunarjea kuangalia tulipokosea na kurekebisha makosa kwa ajili ya mchezo ujao wa ligi kuu,” alisema Lazaro.
