Na mwandishi wetu
Mabingwa watetezi wa Kombe la Mapinduzi, Simba SC wamepangwa Kundi C pamoja na timu za Mlandege na KVZ katika michuano hiyo inayotarajia kuanza Januari Mosi, mwakani kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Wakati Simba wakipangwa kundi hilo, kundi linaloonekana kuvuta hisia za wengi ni Kundi B ambalo linazikutanisha timu mbili kutoka Ligi Kuu ya NBC za Yanga na Singida Big Stars pamoja na KMKM kutoka Zanzibar inakofanyika michuano hiyo.
Makundi mengine mawili yaliyosalia ni Kundi A linaloundwa na Azam waliotinga fainali michuano iliyopita kabla ya kufungwa na Simba kwa bao 1-0, ikiwa sambamba na Malindi na Jamhuri. Kundi D linaundwa na Namungo, Chipukizi na Aigle Noir ya Burundi, timu pekee mshiriki nje ya Tanzania.
Aidha, Mwenyekiti wa kamati ya michuano hiyo, Khamis Abdallah Said amefafanua kuwa safari hii kila kundi itapita timu moja itakayomaliza kinara na hatua itakayofuata itakuwa ni nusu fainali.
Nusu fainali ya kwanza itapigwa Januari 8 ikizikutanisha kinara wa Kundi A dhidi ya kinara wa Kundi B wakati nusu fainali ya pili itachezwa Januari 9 baina ya kinara wa Kundi C dhidi ya kinara wa Kundi D. Mechi ya fainali inatarajiwa kupigwa Januari 13, mwakani.
Simba ililibeba taji hilo katika michuano iliyopita baada ya kuichapa Azam bao 1-0 ikineemeka kwa bao la Medie Kagere aliyefunga kwa mkwaju wa penalti baada ya Pape Sakho kuchezewa rafu katika eneo la penalti.
Kagere ambaye alikuwa kinara wa mabao akiwa na Simba, katika michuano hii atashiriki akiwa na timu ya Singida Big Stars.
Soka Simba, KVZ kundi moja Mapinduzi Cup
Simba, KVZ kundi moja Mapinduzi Cup
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
