Na mwandishi wetu
Baada ya kuiongoza Simba kwa mara ya kwanza katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kocha Juma Mgunda amesema hana hofu na hilo kwani anajivunia ubora wa wachezaji wake.
Mgunda anatarajia kuweka rekodi ya kushiriki hatua hiyo kama kocha kupitia Simba ambayo imepangwa Kundi C ambalo pia lina timu za Raja Casablanca ya Morocco, Horoya AC ya Guinea na Vipers ya Uganda.
Katika miaka minne iliyopita, Simba imekuwa na rekodi nzuri kwenye hatua hiyo kwa kufanya vizuri na kutinga robo fainali.
Mgunda ameiambia GreenSports kuwa: “Kusema woga itakuwa si lugha nzuri kwenye mpira, hakuna woga ni kuheshimu, ni mara yangu ya kwanza kwenye hatua hii kama ilivyokuwa mwanzo wakati tunapambana kuingia makundi.
“Sasa tumeingia na ni mara yangu ya kwanza lakini najivunia wachezaji nilionao ambao wengi wao hii si mara ya kwanza, kwahiyo inaonesha ni jinsi gani tukijiandaa, tukijipanga vizuri nina hakika mwisho wa yote kwa uweza wa Mungu tutafanya vizuri.”
Mgunda ambaye ametua Simba akitokea Coastal Union Septemba, mwaka huu kurithi mikoba ya Zoran Maki pia amewataka viongozi, benchi la ufundi na mashabiki kuungana pamoja ili kuhakikisha wanashinda pamoja kwenye hatua hiyo ngumu.
Aliongeza kuwa timu wanazokutana nazo ni ngumu na zina historia nzuri hivyo mara moja wataanza kazi ya kujua watacheza vipi, wafanye nini na wakiwa ugenini wajipambanue vipi kutokana na uhalisia wa ushindani wa timu hizo na hakutakuwa na mechi rahisi.
Katika mechi za awali za kufuzu makundi, Mgunda aliiongoza Simba kuibomoa Big Bullets ya Malawi kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-0 kabla ya kuitungua Primeiro de Agosto ya Angola kwa mabao 4-1 na kutinga makundi.
LigiKuu Mgunda: Sina hofu Ligi ya Mabingwa
Mgunda: Sina hofu Ligi ya Mabingwa
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
