Madrid, Hispania
Baba katoka Real Madrid kaingia mtoto. Enzo Alves ambaye ni mtoto wa beki wa zamani wa Real Madrid, Marcelo amesaini mkataba wa kwanza na klabu hiyo.
Enzo mwenye umri wa miaka 13 sasa amekuwa katika akademi ya klabu hiyo tangu mwaka 2017 na amethibitisha kusaini mkataba huo kupitia mtandao wa Instagram aliposema, “Mkataba wa kwanza na klabu bora duniani, nina furaha sana.”
Enzo ni mshambuliaji ambaye ameanza kupewa sifa za kutamba hapo baadaye akiwa anaichezea timu ya watoto chini ya miaka 14 ya klabu hiyo akisajiliwa kupitia kampuni ya wakala wa michezo ya Group Doze ambayo imeanzishwa na baba yake.
Baada ya kuichezea Real Madrid kwa takriban miaka 15, Marcelo aliondoka Real Madrid Majira ya Kiangazi mwaka huu na kujiunga na Olympiakos ya Ugiriki akimuacha mwanawe, Enzo katika akademi ya klabu hiyo.
Katika kipindi chote hicho akiwa na klabu hiyo kongwe ya Hispania, amebeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tano na taji la La Liga mara sita.
Katika msimu wake wa mwisho alibeba taji la Ligi ya Mabingwa na lile la La Liga akiwa nahodha ingawa nafasi yake kikosi cha kwanza ilianza kuwa finyu bado ameacha rekodi ya kuwa mchezaji aliyeweka historia ya kubeba mataji mengi, 25, akiwa na klabu hiyo.
Marcelo hata hivyo amekuwa na wakati mgumu nchini Ugiriki akiishia kucheza mechi mbili za Super League msimu huu, mechi ambazo pia ameingia akitokea benchi.
Kimataifa Mtoto wa Marcelo asaini Real Madrid
Mtoto wa Marcelo asaini Real Madrid
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
