Doha, Qatar
Majanga yanazidi kuiandama Brazil kabla ya mechi yake ya robo fainali na Korea Kusini, ikiwa bado haijajua hatma ya nyota wake Neymar, wachezaji wengine wawili, Gabriel Jesus na Alex Teles ni majeruhi na wameondolewa katika kikosi cha timu hiyo.
Ukiacha wachezaji hao, majeruhi wengine katika kikosi cha Brazil ni Danilo na Alex Sandro japo yapo matumaini kwamba huenda wakawa fiti kuivaa Korea Kusini kesho, Jumatatu.
Shirikisho la Soka Brazil (CBF) jana Jumamosi lilitoa taarifa ya kuondolewa kwa Jesus na Teles katika mechi zilizobaki za timu hiyo baada ya kuumia katika mechi yao ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya Cameroon, mechi ambayo Brazil ililala kwa bao 1-0.
Telles alitolewa dakika ya 54 na Jesus kujikuta akilazimika kutoka uwanjani dakika 10 baadaye hali ambayo inazidi kuongeza majanga katika timu hiyo kwani bado haijawa na uhakika kuhusu nyota wake Neymar ambaye aliumia enka ya mguu wa kulia katika mechi ya kwanza ya timu hiyo ya hatua ya makundi dhidi ya Serbia, mechi ambayo Brazil ilishinda kwa mabao 2-0.

“Wachezaji Alex Telles na Gabriel Jesus wamefanyiwa vipimo Jumamosi asubuhi wakiwa pamoja na daktari wa timu Rodrigo Lasmar, vipimo vimeonyesha ukubwa wa majeraha kwenye magoti ya mguu wa kulia na hakuna uwezekano wa kupona kwa wakati na kuendelea kushiriki fainali za Kombe la Dunia za Qatar 2022,” ilieleza taarifa ya CBF
Kuumia kwa wachezaji hao linakuwa pigo si kwa Brazil tu bali hata klabu zao, Jesus ambaye pia ni mshambuliaji wa Arsenal inayoshika usukani katika Ligi Kuu England na inahitaji kumtumia mara baada ya fainali za Kombe la Dunia kama ilivyo kwa Telles ambaye anaichezea Sevilla kwa mkopo akitokea Manchester United.
Brazil wakati huo huo inaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya Neymar ambaye kwa mara ya kwanza tangu aumie jana Jumamosi alifanya mazoezi na wachezaji wenzake kabla ya kuendelea na mazoezi maalum peke yake akiwa katika uangalizi mwalimu wa viungo, Ricardo Rosa.
