Doha, Qatar
Baada ya Ghana kushindwa kufuzu hatua ya mtoano kwenye fainali za Kombe la Dunia, kocha wa timu hiyo, Otto Addo ametangaza kung’atuka katika nafasi hiyo.
Addo mwenye umri wa miaka 47 alikabidhiwa jukumu la kuinoa timu hiyo, Februari mwaka huu baada ya kutimuliwa kwa kocha Milovan Rajevac kwa makubaliano ya kuwa kocha wa muda aliyepewa mkataba hadi mwishoni mwa Desemba.
Kocha huyo hata hivyo pamoja na kupewa jukumu hilo bado alikuwa akifanya kazi ya kocha wa kukuza vipaji katika klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani.
“Wakati wote nilikuwa nikisema kwamba hata kama tutafuzu kwenye Kombe la Dunia nitang’atuka. hata kama tukiwa mabingwa wa dunia pia, mimi na familia yangu tunaiona kesho yetu nchini Ujerumani,” alisema Addo.
Katika fainali za Kombe la Dunia, Ghana ilikuwa Kundi H na licha ya kuifunga Korea Kusini lakini ilishindwa kutamba mbele ya Ureno na Uruguay na kujikuta ikishika mkia katika kundi hilo na hivyo kushindwa kusonga mbele.
“Soka ni mchezo mzuri, japo kuna wakati unakuwa mbaya, mbaya kwetu leo (majuzi) nina hakika tutajifunza katika hili kwa ajili ya siku zijazo,” alisema.
Addo alizaliwa katika jiji la Hamburg nchini Ujerumani na wazazi wake wakiwa wanatokea nchini Ghana na ameishi Ujerumani na kucheza soka nchini humo kabla ya kuigeukia kazi ya ukocha ambayo anaendelea kuifanya nchini Ujerumani.
Kimataifa Kocha Ghana ang’atuka
Kocha Ghana ang’atuka
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
