Doha, Qatar
Mshambuliaji wa Uruguay, Luis Suarez amesema hatoomba radhi kwa tukio la kuunawa mpira ambalo liliwanyima Ghana nafasi ya kufikia nusu fainali ya Kombe la Dunia 2010 licha ya kuambiwa kwamba anaonekana kama shetani nchini Ghana.
Leo Ijumaa jioni, Ghana inacheza na Uruguay, mechi ya Kundi ya H ya fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea Qatar huku moja ya mambo yanayozungumzwa kuelekea mechi hiyo ni tukio hilo la Suarez ambaye aliunawa mpira uliokuwa upigwe kichwa na Dominic Adiyiah na matarajio ya mashabiki wengi hasa wa Ghana ni kwamba mpira ule ungekwenda wavuni.
Baada ya tukio hilo, Ghana walipewa penalti wakati matokeo yakiwa sare ya bao 1-1 lakini mkwaju wa uliopigwa na Asamoah Gyan uligonga mwamba na hatimaye mchezo kumalizika kwa sare kabla ya timu hizo kupigiana penalti ambapo Uruguay ilishinda kwa penalti 4-2 na kukutana na Uholanzi katika hatua ya nusu fainali.
Tukio hilo liliendelea kuwa gumzo na kuonekana kama Suarez ndiye aliyeinyima Ghana nafasi ya kuwa timu ya kwanza ya Afrika kufikia hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia.
Suarez alipoulizwa na mwandishi wa habari wa Ghana kuhusu tukio hilo na namna anavyoonekana kama shetani nchini Ghana, alisema kwamba yeye hapaswi kulaumiwa kwa Ghana kushindwa kufikia nusu hatua ya fainali.
“Siwezi kuomba radhi kuhusu tukio hilo, kweli niliushika mpira lakini mchezaji alikosa penalti, si mimi, ningeomba msamaha kama ningecheza rafu na kupewa kadi nyekundu lakini katika tukio lile nilipewa kadi nyekundu na mwamuzi akasema ipigwe penalti,” alisema.
“Si kosa langu, mimi si niliyekosa penalti, mchezaji aliyekosa penalti alisema angeweza kufanya hivyo hivyo katika mazingira yale, kwa hiyo katika suala hilo halikuwa jukumu langu,” alisema mchezaji huyo ambaye pia aliwahi kufungiwa miezi minne kwa kumng’ata beki wa Italia, Giorgio Chiellini wakati akiichezea Uruguay kwenye fainali za Kombe la Dunia 2014.
“Wanasema mimi ni shetani na mambo mengine lakini nini nilichofanya kwa Chiellini, niliendelea kucheza dhidi yake baada ya hapo, nilifanya kosa na tulishikana mikono, huwezi kukaa unafikiria mambo yaliyopita na kulipa kisasi kwa sababu hiyo haiwezi kukusaidia,” alisema.
Kwa Suarez inatarajiwa kwamba huenda akastaafu soka la kimataifa iwapo Uruguay itashindwa kupata matokeo mazuri katika mechi na Ghana ingawa amesema kwamba anakiamini kikosi chao kiko vizuri na kitaibuka na ushindi.
Mechi za leo Ijumaa, Kombe la Dunia
Kundi G
Cameroon v Brazil, saa 4:00 usiku
Serbia v Switzerland, saa 4:00 usiku
Kundi H
Ghana v Uruguay, saa 12:00 jioni
Korea Kusini v Ureno, saa 12:00 jioni
