Doha, Qatar
Kiungo wa Brazil, Casemiro leo Jumatatu amefunga bao muhimu dhidi ya Switzerland na kuiwezesha timu yake kufuzu hatua ya mtoano ya fainali za Kombe la Dunia wakati Ghana ikipambana kishujaa na kuibwaga Korea Kusini kwa mabao 3-2.
Bao pekee la Casemiro lilipatikana dakika saba kabla ya kutimia dakika tisini baada ya kufumua shuti la mguu wa kulia na mpira kumgusa kidogo beki mmoja wa Switzerland na kujaa wavuni pembeni huku kipa wa Switzerland, Yann Sommer akiwa anauangalia mpira huo asijue la kufanya.
Kabla ya bao la kiungo huyo wa Man United, Brazil ilipata bao kupitia kwa Vinicius Jr kwa shuti la chinichini akitokea upande wa kushoto lakini baada ya mwamuzi kuangalia picha za VAR alilikataa bao hilo kwa madai kuna mchezaji wa Brazil aliotea.
Nao Switzerland kwa muda mrefu walionyesha utulivu na kuvuruga mipango ya Brazil iliyojaa mafundi na kuibua dalili za mechi kumalizika kwa sare kabla Casemiro hajafanya yake na kuifanya Brazil iwe imeshinda mechi mbili na moja kwa moja kufuzu hatua ya mtoano.
Baada ya Brazil kufuzu ikiwa kinara wa Kundi G sasa kazi ipo kwa Switzerland iliyoshinda mechi moja na kupoteza moja pamoja na Cameroon na Serbia ambazo zote zina sare moja moja na zimepoteza mechi moja kila moja.
Nao wawakilishi wa Afrika, Ghana walipanbana na kupata ushindi katika mechi ya Kundi H baada ya kuwaliza Korea Kusini kwa mabao 3-2 wakiwa wa kwanza kupata bao dakika ya 24 lililofungwa na beki wa Southampton, Mohammed Salisu na kuongeza la pili dakika 10 baadaye mfungaji akiwa ni nyota wa Ajax, Mohammed Kudus.

Korea Kusini ikishangiliwa kwa nguvu na mashabiki wake ilipata bao la kwanza dakika ya 58 mfungaji akiwa Cho Gue-sung na dakika tatu baadaye, Cho Gue-sung ambaye pia ni mfungaji bora wa ligi ya Korea Kusini kwa mara nyingine aliifungia timu yake bao la kusawazisha lakini alikuwa ni Kudus aliyebadili matokeo dakika saba baadaye na kuifanya Ghana itoke kifua mbele.
Ghana sasa inashika nafasi ya pili katika Kundi H ikiwa na pointi tatu, imetanguliwa na Ureno ambayo inacheza na Uruguay jioni hii wakati Korea Kusini inashika mkia na pointi yake moja na haikushangaza kuona baadhi ya wachezaji wake wakilia baada ya mechi yao na Ghana ingawa matokeo ya mechi ya Uruguay na Ureno yanaweza kubadili msimamo wa kundi hilo katika nafasi za juu.
Matokeo ya mechi za Kombe la Dunia leo Jumatatu…
Kundi G
Cameroon 3-3 Serbia
Brazil 1-0 Switzerland
Kundi H
Korea Kusini 2-3 Ghana
